SERIKALI KUJA NA MKAKATI KULINDA MASHAMBA YA MIFUGO
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kuja na mkakati madhubuti wa kulinda shamba la uzalishaji mifugo Mabuki lililopo Misungwi dhidi ya uvamizi ili kuongeza tija kwa kuzalisha mbegu bora zitakazoendana na mahitaji ya soko.
Akizungumza wakati wa ziara katika shamba la uzalishaji mifugo Mabuki iliyofanyika Desemba 29, 2025, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani amesema serikali imejipanga kuja na mkakati wa kukabiliana na wavamizi wa shamba la mifugo Mabuki na kutoa rai kwa wananchi kulinda rasilimali hiyo ya umma.
" Tumekuwa na ripoti mbalimbali za wananchi kuingiza mifugo yao katika shamba hili (Mabuki) hivyo kusababisha kusambaza magonjwa mpaka kwenye mifugo yetu na kuharibu mashamba ya malisho yaliyokwisha pandwa, rai yangu kwa watanzania wenzangu, hasa wale tunaoishi karibu na shamba hili tunapofanya mwingiliano huu tuna haribu vizazi vya mbegu vilivyopo" alisema Mhe. Kamani.
Aidha, alisema Wizara imeshaanza kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama ili kupata usaidizi zaidi wa kulinda mashamba ya mifugo jambo litakalofanikisha kutimiza adhma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya wafugaji.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Uzalishaji mifugo Mabuki Bi. Lina Mwala Amesema kwa kipindi cha miaka mitano uzalishaji katika shamba hilo umeongezeka kutoka ng'ombe 1,900 hadi kufikia ng'ombe 2,500 licha ya changamoto zinazolikabiri shamba hilo .
Ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani imelenga kukagua shughuli za uzalishaji katika shamba la mifugo Mabuki, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania, Wakala ya Mafunzo ya Mifugo, TVLA, ZVC pamoja na kuzungumza na watumishi.