DKT. BASHIRU AWATAKA VIJANA (BBT) KUTUMIA VEMA FURSA WALIYOPEWA NA SERIKALI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka vijana wanaonufaika na programu ya “Jenga kesho iliyo bora” (BBT) waliopo kwenye ranchi ya Kagoma mkoani Kagera kutumia vema fursa uwekezaji uliowekwa na Serikali kwenye programu hiyo.
Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo Desemba 30,2025 mara baada ya kufika kwenye ranchi hiyo kwa lengo la kukagua maendeleo ya programu hiyo ambapo amewaeleza kuwa wao ni nguzo kuu ya Maendeleo nchini.
“Mhe. Rais ameelekeza mpewe zaidi ya hekta 700 kwa miaka 5 bila kulipa hata shilingi kwa ajili ya ada ya pango na kwa ukubwa wa eneo lenu kila mwaka mlipaswa kulipa shilingi milioni 9 hivyo kwa miaka 5 maana yake mmepewa ruzuku ya Serikali ya milioni 45 na tunaelekea kupandisha kodi maana yake itakuwa zaidi ya hapo” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa mbali na ruzuku hiyo Serikali imewawezesha vijana hao mkopo usio na riba wa zaidi ya Sh. Bil. 1 huku pia ikiwawezesha pikipiki 2, kisima kirefu cha maji na mfumo wa umeme wa nishati ya Jua.
“haya yote akiwezeshwa mtu mwingine ambaye ni mjasiriamali baada ya miaka 5 atakuwa ni bilionea ambaye ameshalipa mkopo wote na amefanya mambo makubwa hivyo jitahidini kufanya kazi kwa nidhamu, uaminifu na ubunifu ili huu uwekezaji uweze kuendelea” Amehitimisha Balozi Dkt. Bashiru.
Kabla ya kuzungumza na vijana hao Balozi Dkt. Bashiru alikagua miundombinu mbalimbali inayotumiwa na vijana hao kwenye ufugaji huku pia akisikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye utekelezaji wa programu hiyo.