​ULEGA AZINDUA TELEVISHENI MTANDAO YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

Imewekwa: Saturday 11, June 2022

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezindua televisheni mtandao itakayobeba maudhui yanayohusu sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi inayojulikana kama “Voice of Agriculture” tukio lililofanyika jana (07.06.2022) kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye hoteli ya Dodoma.

Mhe. Ulega amebainisha kuwa televisheni hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kuhusu teknolojia mbalimbali zinazotekelezwa kupitia sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo amewataka waendeshaji wa televisheni hiyo kuhakikisha wanakuwa na maudhui yenye kuwavutia watazamaji wakati wote.

“Ni watu wachache wanaokuwa na fikra kisha wakazifanyia kazi fikra hizo na hao ni watu wa kuwapongeza sana hivyo naomba nitumie fursa hii kumpongeza dada Elizabeth na timu yake yote kwa kufikiria na kuja na ubunifu huu wa kuunganisha maudhui ya Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi” Amesema Mhe. Ulega.

Mhe. Ulega amesema kuwa uwepo wa Televisheni hiyo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya kwa vijana ambapo ameongeza kuwa hatua hiyo ni matokeo makubwa ya kifikra na kiuwekezaji.

“Najua kwa kuanzia haitakuwa kazi rahisi lakini ni naomba mjitahidi sana kwenye uzalishaji kuwe na ubunifu wenye kuvutia ili msiwachoshe watazamaji kwa sababu wakianza tu kulalamika mtapunguza watazamaji na kwa sababu huwa wanapatikana kwa mbinde sana itawasumbua kuwarejesha tena” Amesema Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa hivi sasa ni wakulima kufanya uzalishaji usio na tija hivyo licha ya mikakati kadhaa ambayo Wizara yake imeiweka, anaamini televisheni hiyo itawasaidia kutoa elimu kuhusu mbinu mbalimbali za kilimo ili waweze kuwa na tija kwenye uzalishaji wao.

“Sisi kama Wizara ya Kilimo tumefarijika sana na tutaitumia “forum” hii kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa sababu miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima wetu ni kutofikiwa kwa kiwango kikubwa na elimu kuhusu kanuni bora za kilimo” Amesema Mhe. Mavunde.

Mhe. Mavunde ameongeza kuwa mpaka sasa kiasi cha mahitaji ya maafisa ugani kwa upande wa sekta ya kilimo hapa nchini ni takribani 20,000 na maafisa ugani waliopo ni 7604 pekee hivyo uwepo wa Televisheni hiyo ni miongoni mwa njia watakazotumia kufikisha elimu ya kilimo kwenye maeneo ambayo hayana maafisa ugani.

Naye Mmiliki wa Televisheni hiyo, Elizabeth Swai amesema kuwa alipata wazo la kuanzisha Televisheni hiyo baada ya kugundua kuna ombwe la mawasiliano baina ya wadau waliopo kwenye sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo imemchukua takribani miaka 5 kukamilisha suala hilo.

“Mimi ni mkulima na ni mfugaji na nimekuwa kwenye hizo sekta kwa zaidi ya miaka 16 sasa hivyo baada ya kugundua ombwe lililopo baina yetu na wataalam na Serikali kwa ujumla ndipo nilipopata wazo la kuanzisha televisheni hii na nimetumia fursa hiyo kuunga mkono juhudi kubwa za Serikali zilizofanywa kwa upande wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi” Amesema Swai.

Uzinduzi wa Televisheni hiyo ni moja ya mambo yaliyoambatana na Mkutano wa 8 wa wachambuzi wa Sera za Kilimo, Mifugo na Uvuvi uliofanyika kwa siku 3 kuanzia juni 6 mwaka huu.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022