RUBAMBAGWE IKAMILIKE MACHI 30-DKT. BASHIRU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameeelekeza mradi wa kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Rubambagwe kilichopo Chato mkoani Geita kikamilike ifikapo Machi 30,2026.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo mara baada ya kufika na kukagua kituo hicho Januari 05,2026 ambapo ameonesha kushangazwa na hali ya kutoendelea kwa shughuli za ujenzi kituoni hapo pamoja na kutengwa kwa fedha zilizopangwa kutekeleza shughuli hiyo.
“Kwa mkandarasi ambaye ana “tight schedule” ya kazi nyingi kama ninavyoziona hapa kungekuwa na shughuli zinazoendelea lakini sioni Cement, kokoto wala shughuli yoyote” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Kufuatia hali hiyo Balozi Dkt. Bashiru amemwelekeza Mhandisi wa Wizara hiyo Bw. George Kwandu kuwasilisha nakala za mpango wa utekelezaji wa awamu ya pili ya ujenzi huo ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mbunge, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Chama cha Mapinduzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili wafuatilie kwa kila wiki hatua kwa hatua ujenzi wa Taasisi hiyo na kuhakikisha unakamilika katika tarehe tajwa.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amemwelekeza Mkuu wa mkoa huo Mhe. Martin Shigela na kamati ya Usalama ya Mkoa huo kufuatilia utekelezaji wa mpango kazi huo kulingana na fedha zinazotolewa na Serikali kwenye mradi huo.