MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI NI JUKUMU LETU-KAMANI
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi kamani amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha sekta binafsi inapiga hatua katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo kwa ujumla.
Mhe. kamani amesema hayo wakati wa ziara yake ya kuitembelea kampuni inayojihusisha na uzalishaji wa kuku wa mayai na nyama ya Lake Zone Farm iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza Januari 06,2026 ambapo amesisitiza Serikali itaendelea kusukuma juhudi za sekta binafsi katika ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Tunajua tunapofanya hivyo tunasaidia kuwanyanyua na wengine ambao kupitia nyinyi watajifunza hiki mnachofanya hivyo naamini tukiendelea na ubunifu huu na sisi kama Wizara tukasaidia kushusha gharama za chakula cha tutarahisisha zaidi mazingira ya wafugaji wetu wa kuku kupata chakula cha kutosha kwa gharama nafuu na kwa misingi hiyo hata bidhaa mtakazopeleka kwenye jamii zitapatikana kwa gharama nafuu pia” Ameongeza Mhe. Kamani.
Aidha Mhe. Kamani ametoa rai kwa wafugaji wakubwa kutengeneza mfumo wa kuwashirikisha na kuwanyanyua wafugaji wengine jambo ambalo anaamini litaongeza tija kwenye ufugaji na kunyanyua jamii zinazowazunguka wafugaji hao.
“Bado tunahitaji wazalishaji wengi zaidi kwa sababu mahitaji ya protini kwenye Mifugo ni makubwa na ndio maana hapa unaona pamoja na kuwa na kuku wengi bado ikifika muda wa kuwauza wale waliohitimisha muda wa kuzalisha mayai bado hupati shida ya soko” Ameongeza Mhe. Kamani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi. Joyce kabago ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuagiza vifaa vya kufugia kuku bila tozo na kuwawezesha wataalam ambao huwatembelea na kuwapatia huduma stahiki.