UIMARISHWAJI WA TVLA UNAENDA KUSAIDIA KUIMARIKA KWA MIFUGO NCHINI KUWEZA KUPATA MASOKO NJE YA NCHI-PROF.SHEMDOE

Imewekwa: Friday 19, May 2023

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amefanya ziara kutembelea Maabara za Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kufahamu na kujionea kazi ambazo zinafanywa na Wakala hiyo.

Akizungumza wakati wa Ziara yake leo Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema uimarishwaji wa TVLA unaenda kusaidia kuimarika kwa mifugo nchini na kuweza kupata masoko mengi nje ya nchi.

Amesema TVLA wamekuwa wakifanya maandalizi ya utengenezaji wa chanjo mbalimbali za mifugo ambazo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali kwenye mifugo.

"Miaka michache iliyopita tulikuwa tunapeleka nyama nje ya nchi tani elfu moja, lakini sasa mwaka huu ambao tunamalizia mwaka wa fedha tayari tumeshavuka tani elfu 12, kwahiyo tunapoelekea ni mahala pazuri". Amesema Prof. Shemdoe.

Aidha amewapongeza TVLA kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ikiwemo kutambua magonjwa ya mifugo ambayo yapo nchini ili kuweza kuyazuia na kuyatokomeza.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha ambazo zimesaidia kuimarisha TVLA na kuweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kuhakikisha wanadhibiti magonjwa ya mifugo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amesema kuwa wanategemea kwa kiasi kikubwa ziara ya Katibu Mkuu kuzaa matunda kwani ameona ni kwa namna gani TVLA wamekuwa wakijtahidi kuhakikisha inafanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake.

Pamoja na hayo amemuhakikishia Katibu Mkuu kuwa wataendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi katika kuhakikisha wanadhibiti magonjwa ya mifugo nchini.

.