NAIBU KATIBU MKUU UVUVI AAGIZA MIUNDOMBINU YOTE YA BANDARI KILWA MASOKO KUFANYIWA MAJARIBIO YA MWISHO MARA MOJA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agnes Meena, ameagiza kukamilishwa mara moja kwa shughuli za upimaji na uingizaji katika matumizi (Testing and Commissioning) ya miundombinu yote ya mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, ndani ya juma lijalo kutoka sasa, ili kuwezesha kuanza kutumika kwa wakati uliopangwa.
Prof. Sheikh ametoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 98.9 ya ukamilishaji, leo 06 Juni 2026, Kilwa mkoani Lindi.
Katika ziara hiyo, Prof. Sheikh alikagua maeneo mbalimbali ya mradi ikiwemo mtambo wa kuzalisha barafu, vyumba vya ubaridi, eneo la kufanyia maandalizi ya samaki, jengo la kupoozea umeme, miundombinu ya kiutawala, karakana ya kutengeneza meli pamoja na gati la kuegeshea meli.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Prof. Sheikh alisema ni muhimu kuhakikisha mifumo na vifaa vyote vinafanyiwa upimaji wa kina na kuthibitishwa utayari wake wa kufanya kazi kwa ufanisi kabla ya kuanza kutumika rasmi.
“Fanyeni kazi masaa 24 kuhakikisha hatua zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na shughuli zote za upimaji na uingizaji katika matumizi zikamilike, ili mradi uweze kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa,” alisema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya China Harbour Engineering Company Ltd (CHEC), Chen Zhifeng, alisema kazi zilizobaki ni chache na zinahusisha ukamilishaji wa baadhi ya marekebisho madogo, usafi wa maeneo yaliyokamilika pamoja na majaribio ya mwisho ya mifumo mbalimbali ya mradi.
Naye Mkurugenzi wa Kuendeleza Miundombinu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo kwa upande wa Wizara, Mhandisi George Kwandu, alisema maendeleo ya utekelezaji wa mradi yanaridhisha na kwamba usimamizi unaendelea kufanyika kwa karibu ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa kuzingatia viwango vya ubora na muda uliopangwa.
Mradi huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli za sekta ya uvuvi kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao ya uvuvi, kuboresha miundombinu ya huduma za uvuvi na kuongeza thamani ya mazao hayo kabla ya kufikishwa sokoni.