SERIKALI YATOA ONYO DHIDI YA UVAMIZI WA ARDHI YA MIFUGO NCHINI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametoa onyo kwa wananchi wanaovamia ardhi ya Karantini ya Mifugo yenye ukubwa wa ekari 2,176 iliyopo Makuyuni, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, akisisitiza kuwa eneo hilo lilitengwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa onyo hilo leo Juni 6, 2026, baada ya kutembelea na kukagua eneo hilo na kueleza kuwa kati ya eneo hilo, ekari 510 tayari zimetolewa kwa Halmashauri ya Monduli kwa ajili ya upanuzi wa Mji wa Makuyuni pamoja na ujenzi wa machinjio ya kisasa yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa halmashauri hiyo.
“Tunataka kutumia maeneo yetu kufanya maendeleo ya kisasa ya sekta ya mifugo, wapo baadhi ya watu wanaochochea migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Ardhi ya mifugo iliyotengwa inapaswa kutumika kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya mifugo kisasa,” amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Isaac Joseph, alisema kuwa wakazi wengi wa Monduli wanategemea shughuli za ufugaji, hivyo wameomba sehemu ya eneo hilo ili kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimath, alisema kuwa asilimia 80 ya shughuli za kiuchumi katika wilaya hiyo zinategemea ufugaji na kubainisha kuwa miongoni mwa changamoto anazoshughulikia ni migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ambapo amependekeza kikundi cha wanawake 90 wa Kijiji cha Makuyuni kipatiwe eneo kwa ajili ya uzalishaji wa malisho.
Akijibu ombi la wananchi la kupewa sehemu ya eneo hilo, Balozi Dkt. Bashiru alisema Serikali itafanya tathmini ili kubaini matumizi bora ya eneo husika lakini haitaruhusu matumizi holela ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mifugo kutumika kwa shughuli zingine.
“Wafugaji furaha yao, maendeleo yao ni mifugo, tusiwanyanyapae wafugaji na wafugaji fuateni sheria, haiwezekani kila ardhi ya mifugo ikatumika kwa huduma nyingine za kijamii tutapoteza maeneo muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo,” alisisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Waziri Balozi Dkt. Bashiru yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya Siku mbili inayolenga kukagua utekelezaji wa sekta za mifugo na uvuvi ambapo msisitizo wake umekuwa kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mifugo ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi, ajira na ustawi wa wananchi.