Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

TUTAONDOA MIZIZI YOTE KWENYE UVUVI HARAMU-DKT. BASHIRU

Imewekwa: 03 January, 2026
TUTAONDOA MIZIZI YOTE KWENYE UVUVI HARAMU-DKT. BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inaondoa mizizi yote inayosababisha vitendo vya uvuvi haramu nchini.

Balozi Dkt. Bashiru amebainisha hayo Januari 03,2026 wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wavuvi kwenye mialo ya Marehe, Rubafu na Kemondo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera ambako alianza kwa kupokea maoni ya wavuvi hao yaliyolenga kutafuta suluhu ya kuondokana na changamoto ya Uvuvi haramu.

“Nyie mnazungumza viwanda vya nyavu lakini vyandarua vya kudhibiti malaria navyo vimeanza kwenda kutumika kuvua samaki kwa hiyo mizizi imeshakuwa mikubwa ni lazima tunoe mashoka na tutakapoanza kunyanyua mashoka hayo tusije tukapoteana” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amewataka wavuvi wote nchini kuwa na mshikamano kwenye ulinzi wa rasilimali za Uvuvi na kupambana na wale wanarudisha nyuma jitihada hizo.

“Nisingependa kuwa Waziri wa kufilisi wavuvi na kuzua taharuki, kila jambo tutalifanya kwa kuwashirikisha kama navyoendelea kufanya na lile lisilo na manufaa hatutalifanya ila lenye manufaa hatutaogopa kulifanya hata kama litakuwa linamkera mtu mwenye nguvu za aina gani” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.

Dkt. Bashiru ametoa tamko hilo kufuatia baadhi ya maoni ya wadau wa Uvuvi kutoka Mwalo wa Marehe walioitaka Serikali kuanza kwa kuzuia uingizwaji wa zana zinazochochea Uvuvi haramu na kuwachukulia hatua za kisheria wauzaji wote wanaoingiza zana hizo nchini.

Awali akitoa maoni yake mbele ya Balozi Dkt. Bashiru mara baada ya kufika eneo la Rubafu mtaalam wa ukuzaji viumbe maji kutoka sekta binafsi Bi. Renata Elias ametoa rai kwa wataalam wa Uvuvi kuondoa urasimu na kupunguza vikwazo kwenye tasnia hiyo ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kwenye tasnia hiyo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo