TUTAJENGA VITUO ATAMIZI NCHI NZIMA-SILINDE

Imewekwa: Friday 19, May 2023

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaweka programu ya atamizi katika mikoa yote nchini kwa mwaka ujao wa fedha.

Mhe. Silinde ameyasema hayo Mei 18, 2023 wakati akitoa salamu za Wizara yake kwenye mwendelezo wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango aliyoifanya eneo la Ngaramtoni mkoani Arusha.

"Mhe. Makamu wa Rais, sasa hv wewe pamoja na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mmejikita katika kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia sekta za uzalishaji na mmefanya hivyo kwenye Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi na kwa upande wa Wizara yetu mnataka Tanzania ibadilike kwenda kwenye ufugaji wa kisasa" Amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde ameongeza kuwa moja ya njia ambazo Serikali inatarajia kutekeleza azma hiyo ni kupitia programu ya unenepeshaji wa Mifugo ambapo imetoa fedha za kujenga vituo Atamizi nchi nzima.

"Lengo ni tuongeze tija, tuongeze na kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi ili pato la Taifa linalotokana na sekta za Mifugo na Uvuvi lionekane kama ilivyo kwa nchi ya Namibia ambao wana mifugo milioni 4 tu lakini inachangia zaidi ya asilimia 54 kwenye pato la Taifa" Amesisitiza Mhe. Silinde.

Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa kwa upande wa sekta ya Uvuvi serikali inakusudia kubadilisha maisha ya wavuvi nchini kwa kuongeza tija kwenye aina ya mavuvi yanayofanyika kwenye vyanzo mbalimbali vya asili na upande wa ufugaji wa samaki.

"Katika kufanikisha hilo, Serikali imetoa mkopo wa boti 160 usio na riba kwa wavuvi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi" Amehitimisha Mhe. Silinde.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ni miongoni mwa mawaziri wa kisekta waliopo kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayoifanya katika mikoa ya Arusha na Manyara kwa lengo la kukagua na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa mikoa hiyo.

.