Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KAMANI-WAFUGAJI SHIKANENI MKONO NA SERIKALI KUHUSU MAJI

Imewekwa: 20 December, 2025
MHE. KAMANI-WAFUGAJI SHIKANENI MKONO NA SERIKALI KUHUSU MAJI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka wafugaji kote nchini kushirikiana na serikali kujenga mabwawa na kuchimba visima ili mifugo iweze kupata maji ya kutosha.

Naibu Waziri Kamani amebainisha hayo (19.12.2025) wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara katika Wilaya ya Hanang, ambapo amewataka wafugaji kuanzia ngazi ya mtu mmoja hadi vikundi kutekeleza hilo badala ya kuisubiria serikali pekee.

Ameongeza kuwa kwa upande wa serikali itaendelea kuweka bajeti ya kujenga mabwawa na kuchimba visima, japokuwa kuna maeneo ambayo vyanzo vya maji viko karibu ambavyo wafugaji wanaweza kujiwekea mkakati wao wenyewe wa kuchimba visima kwa ajili ya maji ya mifugo yao.

Katika hatua nyingine akiwa katika mnada wa Katesh uliopo wilayani humo, ameagiza Bodi ya Nyama nchini (TMB) kufika kwenye mnada huo ili kujiridhisha miundombinu inayotumika katika eneo la machinjio.

Amebainisha hayo baada ya kutoridhishwa na baadhi ya miundombinu, huku akisisitiza ni muhimu kuhakikisha bidhaa ya nyama inayotoka eneo hilo inakuwa salama ili kulinda afya ya mlaji na kufikia malengo ya serikali kufikia zaidi katika masoko ya kimataifa.

Katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara Mhe. Naibu Waziri Kamani amesikiliza maoni na kero mbalimbali ambazo wafugaji wameziwasilisha kwake na kutoa maelekezo ya muda mfupi na muda mrefu.

Baadhi ya kero ambazo zimezungumzwa zaidi na wafugaji ni kuhusu maji, malisho na migogoro ya ardhi, ambapo amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuhakikisha inamlinda mfugaji na mifugo yake na kwamba waendelee kufuata sheria za nchi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo