TANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA MAPAMBANO DHIDI YA SOTOKA YA MBUZI NA KONDOO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR), ikiwa na dhamira ya kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damasi Kamani (Mb), wakati akihutubia Kikao cha pili cha mwaka cha kundi la ushauri la bara la Afrika kuhusu kutokomeza ugonjwa huo, kilichofanyika jijini Abidjan, Côte d’Ivoire, Novemba 16–17, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kamani amesema ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo ni tishio kubwa kwa usalama wa chakula, kipato cha wafugaji, ajira na biashara ya mifugo, hususan kwa wanawake na vijana wanaotegemea mifugo hiyo kujipatia kipato, na amesisitiza kuwa kutokomeza ugonjwa huo si suala la afya ya wanyama pekee, bali ni hatua muhimu katika kulinda uchumi wa kaya na kuimarisha maendeleo ya taifa.
Aidha, Mhe. Kamani ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza jumla ya Shilingi bilioni 216 katika Kampeni ya Taifa ya Chanjo, Utambuzi na Ufuatiliaji wa Mifugo ya miaka mitano, iliyoanza mwaka 2025/2026, na katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, zaidi ya wanyama milioni 50.4 walichanjwa, wakiwemo mbuzi na kondoo milioni 16.8 kati ya milioni 17.2 waliolengwa kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa Sotoka, sawa na asilimia 97.7 ya lengo lililowekwa.
Vilevile, Mhe. Kamani amesema katika awamu ya pili ya kampeni hiyo, Serikali imetenga Dola za Marekani milioni 13 na tayari imenunua dozi milioni 10.7 za chanjo, huku FAO na AU-IBAR zikichangia jumla ya dozi milioni 2.35, na ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, uwezo wa maabara na utambuzi wa mifugo, pamoja na kushirikiana na nchi jirani kuhakikisha udhibiti wa magonjwa ya mifugo unatekelezwa kwa mfumo wa kikanda.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Kamani amezitaka taasisi za fedha za kikanda na kimataifa kuongeza ushirikiano wa kifedha na kiufundi ili kuharakisha kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika, na amesisitiza kuwa Tanzania inaamini katika kauli mbiu isemayo “Afya ya Wanyama ni Afya ya Kila Mtu,” akibainisha kuwa mafanikio ya mapambano dhidi ya magonjwa ya mifugo yanapaswa kupimwa kwa matokeo halisi kwa wafugaji, usalama wa chakula na ustawi wa jamii.