Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU -TUTATOA BOTI ZA KISASA ZA UVUVI NA TUTAWASHIRIKISHA WAVUVI

Imewekwa: 15 November, 2026
DKT. BASHIRU -TUTATOA BOTI ZA KISASA ZA UVUVI NA TUTAWASHIRIKISHA WAVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally amesema serikali itawashirikisha wadau wa uvuvi wakiwemo wavuvi na viongozi ngazi ya jamii katika mpango wa ukopeshaji wa Boti za Kisasa za Uvuvi ili boti hizo ziwanufaishe wavuvi kulingana na malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Bashiru, amesema hayo baada ya Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe. Nape Nnauye kuibua hoja ya  kupatiwa boti kwa ajili ya uvuvi kwa wananchi wake, hoja aliyotoa wakati wa Mkutano wa Hadhara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi katika ziara yake Mkoani Lindi leo Novemba 14, 2026.

Akijibia hoja ya Mheshimiwa Mbunge, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali imeshatoa boti 240 huku kati ya hizo boti 144 zimegawiwa kwa ukanda wa pwani katika mikoa ya Dar ea Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.

Amesema awamu zilizopita ukopeshaji wa boti ulifanyika lakini serikali imeona haja ya kushirikisha wadau wakiwemo wavuvi katika mpango mzima wa utoaji wa boti hizo ili kukidhi mahitaji ya wavuvi.

Vile vile, Mhe. Dkt. Bashiru amesema katika kuongeza namna ya kunufaika na uvuvi wa bahari Kuu na katika eneo maalum la uchumi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanikisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi eneo la Kilwa Masoko, bandari ambayo itakuwa kichocheo kikuu cha kuongeza thamani sekta ya uvuvi, ambapo ametoa rai kwa wabunge,viongozi na wananchi wote kuanza kuelimishana jinsi ya kunufaika na bandari hiyo.

Amesema bandari hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 280 fedha za ndani ya Nchi, imeshakamilika na sasa ipo tayari kuanza uzalishaji ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua bandari hiyo hivi karibuni.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo