Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

TANZANIA YAANZA KUJADILI USTAWI WA VIUMBE MAJI

Imewekwa: 31 August, 2026
TANZANIA YAANZA KUJADILI USTAWI WA VIUMBE MAJI

Nchi ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Serikali linalohamasisha kampeni ya “AFYA MOJA” (OHD) imeanza mkutano wa siku 2 unaojadili ustawi wa samaki wanaofugwa na  viumbe maji kwa ujumla unaofanyika Agosti 31 hadi Septemba 1,2026 jijini Dar-es-salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amesema kuwa mbali na lengo la kutoa uelewa na kuongeza ufahamu kuhusu ustawi wa samaki na wanyama wa majini mkutano huo pia unalenga kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu afya ya samaki,usalama wa viumbe maji na uzalishaji unaowajibika.

“Tanzania pamoja na Afrika kwa ujumla suala la ukuzaji viumbe maji limeshika kasi na watu wengi wamekuwa wakiwekeza kwenye tasnia hiyo hivyo mkutano huu unaangazia fursa na changamoto zinazoikabili tasnia ya ukuzaji viumbe maji ili kuhakikisha kwamba ufugaji wa viumbe maji unafanyika kwa uadilifu na kwa kuzingatia ustawi” Amesema Bi. Meena.

Aidha Bi. Meena ameongeza kuwa mkutano huo utawapa fursa wadau hao wa Tasnia ya ukuzaji viumbe maji kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendeleza tasnia hiyo kwa kuzingatia maadili na hivyo kufanikisha lengo la kuhakikisha nchi inafuga samaki wenye ubora na afya ili kulinda afya ya mlaji pia.

Kwa upande wake katibu wa chama cha wakuzaji viumbe maji nchini Bw. Jofrey Rucho amesema kwa muda mrefu samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili wamekuwa wakipungua na hivyo kufungua fursa kwa wakuzaji viumbe maji ambao wamekuwa na mwitikio mkubwa kwenye ufugaji wa samaki.

“Kwa hiyo tunataka kuhakikisha yale yote ambayo mkulima anatakiwa kuzingatia ili kukidhi vigezo na ubora wa samaki wanaoenda kuliwa na mlaji wa mwisho kule nyumbani yanaeleweka na kufuatwa” Amesema Bw. Rucho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Serikali linalohamasisha kampeni ya “AFYA MOJA” (OHD) Dkt. Kikiope Oruwarore amesema kuwa Shirika lake kwa kuwa mdau kinara wa tasnia ya ukuzaji viumbe maji barani Afrika,liliona haja ya kuandaa mkutano huo ili kuhakikisha ukuzaji viumbe maji nchini unakuwa endelevu na mazao yanayozalishwa kutokana na tasnia hiyo yanakuwa salama kwa afya ya binadamu.

Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano wa wadau wakiwemo serikali, wafugaji wa samaki, watafiti, taasisi za elimu, sekta binafsi na mashirika ya kiraia, Kujadili sera na kanuni zinazoweza kujumuisha ustawi wa samaki katika mikakati ya kitaifa na kikanda ya ufugaji wa samaki na kuandaa mipango ya utekelezaji ya kukuza mbinu za ufugaji zinazozingatia ustawi wa samaki, usalama na uendelevu.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo