TANZANIA NA QATAR KUONGEZA USHIRIKIANO WA UWEKEZAJI KATIKA MIFUGO NA UVUVI
Serikali ya Tanzania imesema iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Qatar katika kuendeleza fursa za uwekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi, ikiwemo kuongeza uzalishaji na usindikaji wa nyama, kupanua masoko ya bidhaa za mifugo katika nchi za Mashariki ya Kati, kuendeleza sekta ya kuku na kuwekeza katika miundombinu ya uvuvi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, wakati wa mazungumzo yake na Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar, Mhe. Dkt. Khalid bin Mohammad Al Attiyah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Thirty-Five Investment Holding, katika ziara yake ya kikazi nchini Tanzania. Kikao hicho kilichofanyika Agosti 31, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Bi. Agnes Kisaka Meena; Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara.
Akizungumzia biashara ya nyama ya ng'ombe, Waziri Dkt. Kakurwa aliiomba kampuni hiyo kutumia uzoefu wake katika biashara kusaidia Tanzania kufungua na kupanua soko la nyama nchini Qatar na Mashariki ya Kati, akisema Tanzania ina malighafi ya kutosha lakini inahitaji kuimarisha masuala ya viwango, usalama wa chakula na taratibu nyingine zinazohitajika ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nyama katika masoko ya kimataifa na Serikali iko tayari kushirikiana na Qatar katika kushughulikia changamoto hizo na kuimarisha uwezo wa wadau wa sekta kufikia viwango vinavyohitajika.
“Tanzania imeongeza mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka takribani tani 1,000 za metriiki mwaka 2021 hadi karibu tani 15,000 kwa sasa, huku ikilenga kufikia angalau tani 50,000 kwa mwaka. Tanzania tayari inauza nyama katika masoko ya Qatar, Oman, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, Jordan, Hong Kong, Vietnam na Comoro, lakini bado kuna fursa kubwa ya kuongeza mauzo hayo kupitia uwekezaji katika uzalishaji, usindikaji, uongezaji thamani na miundombinu ya usafirishaji wa nyama.” Alisema Waziri Dkt. Kakurwa
Aidha, Mhe. Dkt. Kakurwa alitaja sekta ya kuku kuwa eneo jingine lenye fursa kubwa kwa uwekezaji, akieleza kuwa Serikali imezindua mkakati wa miaka 10 wa kuku unaolenga kuimarisha na kurasimisha zaidi sekta hiyo. Alisema sekta hiyo ina mnyororo mpana wa thamani unaohusisha wazalishaji wadogo na wadau mbalimbali, hivyo kuna fursa katika uzalishaji wa chakula cha kuku, chanjo, pembejeo, kuongeza tija, usambazaji na kuboresha ubora wa malighafi.
Katika sekta ya uvuvi, Waziri Dkt. Kakurwa alisema Serikali inapendekeza kuanzishwa kwa mchakato wa majadiliano kati ya Thirty-Five Investment Holding na Kampuni ya Uvuvi Tanzania (TAFICO), kama ilivyo kwa ushirikiano unaoendelea na NARCO, ili kuweka msingi wa uwekezaji katika sekta hiyo. Alisema uvuvi ni eneo tofauti na shughuli za NARCO, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na MoU maalum kati ya TAFICO na Thirty-Five Investment Holding.
“Tanzania imekamilisha Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, yenye miundombinu ya mnyororo wa baridi, eneo la usindikaji, kituo cha mafuta, kutengeneza barafu, kugandisha na uhifadhi wa baridi. Serikali pia imefanya utafiti wa uwezekano wa kujenga bandari nyingine ya uvuvi Bagamoyo ambapo fursa hizo zinaweza kuhusisha uvuvi wa bahari kuu, hususan jodari, pamoja na usindikaji na uongezaji thamani wa mazao ya uvuvi. Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko imefikia hatua ya juu ya utekelezaji na ina miundombinu ikiwemo mtambo wa kuzalisha barafu, vyumba vya ubaridi, eneo la maandalizi ya samaki na gati la kuegeshea meli.” Alisema Mhe. Dkt. Kakurwa
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Khalid bin Mohammad Al Attiyah alionyesha nia ya kuendelea na majadiliano kuhusu fursa hizo, akitaka kufahamu zaidi kuhusu miundombinu ya uvuvi na namna wawekezaji watakavyoweza kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani. Pia alitolea mfano wa Kesennuma nchini Japan, ambako sekta ya uvuvi ilirejeshwa kwa kiasi kikubwa baada ya kuathiriwa na tsunami ya mwaka 2011, akisisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka uzoefu wa nchi nyingine katika kuendeleza sekta hiyo.