​TANZANIA INAZALISHA TANI 900,000 PEKEE ZA VYAKULA VYA MIFUGO - RAS IRINGA

Imewekwa: Wednesday 01, September 2021

Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyakula vya mifugo vinavyosindikwa viwandani kwa zaidi ya asilimia 60 huku sababu ikitajwa ni idadi ndogo ya Viwanda vikubwa vya usindikaji.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi. Happiness Seneda katika taarifa yake iliyosomwa na mshauri wa mifugo Mkoa wa Iringa, Bw. Mwita Chacha wakati akifunga mafunzo kwa wakaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo Agosti 13, 2021 mkoani Iringa.

Bi. Seneda alisema kwa Sasa Kuna viwanda vya kati na vidogo 185 ambavyo vinazalisha tani 1 hadi 80 kwa siku sawa na wastani wa tani 900,000 kwa mwaka kulinganisha na mahitaji ya tani milioni 2 za vyakula vya mifugo kwa mwaka.

"Viwanda vingi vilivyopo ni vidogo ambavyo hutengeneza vyakula na kuuza kwa bei Kubwa hivyo kulazimisha wafugaji kutengeneza vyakula vyao wenyewe na mara nyingi vimekuwa havina ubora na kukosa viinilishe muhimu vya kukidhi mahitaji ya mifugo" alisema Bi. Seneda.

Hali kadhalika Bi. Happiness Seneda aliwataka wataalam hao kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wafugaji baada ya kubainika baadhi yao kujikita zaidi katika matumizi ya nafaka na rasilimali zisizofaa kwa matumizi ya vyakula vya binadamu na kubadilisha kuwa vya mifugo.

Bi. Seneda alibainisha kuwa hali hiyo imeleta athari kwa mifugo na walaji wa mazao yatokanayo na mifugo kutokana na uwepo wa sumukuvu na madini mazito katika nafaka.

"Katika kuendeleza tasnia ya vyakula, serikali itaendelea kuratibu uzalishaji wa vyakula vya mifugo kwa kusimamia ubora wake kwa kushirikiana na shirika la viwango nchini (TBS) ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wawekezaji kufungua viwanda vya usindikaji wa vyakula vya mifugo" alihitimisha Bi. Seneda

Mafunzo haya yalifanyika kwa muda wa siku mbili ambapo wataalam 16 wamepata mafunzo na kukabidhiwa vyeti lengo likiwa ni kutatua changamoto ya ubora wa vyakula vya mifugo vinavyotumiwa na wafugaji.

.