WAKUZAJI VIUMBEMAJI 2000 KUJENGEWA UWEZO WA MBINU BORA ZA UFUGAJI SAMAKI
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wakuzaji viumbemaji katika uzalishaji wa samaki, kutengeneza chakula cha samaki, usimamizi wa mabwawa na masuala ya jinsia na lishe ili kuimarisha mifumo jumuishi ya usalama wa chakula.
Akizungumza katika kikao kazi cha kutekeleza programu hiyo, leo Januari 15, 2026 wilayani Songea mkoani Ruvuma, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Ruvuma, Bw. Deogratius Sibula amesema programu ya (AFDP), inayotekelezwa kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni nyenzo muhimu ya Serikali katika kuimarisha Sekta ya Ukuzaji viumbemaji nchini.
“Programu hii itafanyika katika halmashauri tano za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Halmashauri za Wilaya ya Mbiga, Namtumbo, Nyasa na Tunduru.” amesema Bw. Sibula
Aidha, Bw. Sibula amesema kuwa Utekelezaji wa Majukumu ya Programu hiyo inalenga kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbemaji 2,000 katika Mkoa wa Ruvuma, ambapo, katika awamu hii utafanyika katika kata 25 ndani ya Halmashauri hizo 5 za Mkoa wa Ruvuma, kuanzia tarehe 15 Januari 2026 hadi tarehe 22 Januari 2026.
Vilevile, Bw. Sibula amebainisha kuwa mafunzo haya ni fursa kwa wakuzaji viumbemaji na yatakuwa na tija kubwa kwa wafugaji wa samaki wa Mkoani Ruvuma na kuhamsha hali ya ufugaji kutoka ule wa kujikimu na kuwa na ufugaji wa kibiashara unaozingatia mbinu bora za ufugaji.
Kwa Upande wake, Afisa Uvuvi Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni Afisa Kiungo wa Programu ya AFDP, Bi. Mkomanile Mahundi amesema zoezi hilo litajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu (PMO) pamoja na wataalam kutoka Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma.
Bi. Mahundi amebainisha kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yataendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Morogoro, Tanga, Geita pamoja na Mkoa wa Tabora