Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU ACHARUKA NARCO KUKOSA DAWA ZA MIFUGO

Imewekwa: 27 February, 2026
DKT. BASHIRU ACHARUKA NARCO KUKOSA DAWA ZA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kushirikiana na Idara ya Huduma ya Mifugo na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa ajili ya kuangalia upatikanaji wa dawa za mifugo kuhudumia ranchi hiyo  iliyopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma na wafugaji wengine kwa ujumla kuzunguka eneo hilo.

Agizo hilo amelitoa leo Februari 26, 2026 wakati akizungumza na kusikiliza changamoto za wafugaji na wawekezaji wadogo waliopewa vitalu ndani ya NARCO Kongwa ambapo Dkt. Bashiru amemwagiza pia Katibu Mkuu wa Wizara yake, kusimamia umoja kwa watendaji pamoja na taasisi zake ili kuiendeleza sekta ya mifugo na uvuvi.

“ Wizara hii ni moja na Waziri wake ni mmoja na aliyemteua Waziri wenu ni Rais huyo mmoja halafu tunashindwa kufanya kazi kama timu moja kwanini?. Watu wa chanjo wako kwenye ofisi yangu, chanjo zinatoka ofisini kwangu, Mkuu wa Madakatari wote wa mifugo yuko kwangu, anayedhibiti dawa za mifugo nchi nzima yuko ofisini kwangu, lakini Ranchi za Taifa, Kampuni yake ambayo nayo ipo ofisini kwangu nayo haina dawa hizo, naelekeza kwa mara ya mwisho jambo hilo, Katibu Mkuu awakumbushe  watendaji ndani ya wizara jukumu lao la kufanya kazi kama timu moja” alisema Balozi Dkt. Bashiru.
 
Hatua hiyo imejiri baada ya Dkt. Bashiru kupokea changamoto kutoka kwa  wafugaji wakiwakilishwa na Bw. Kedmond Maskini ambaye ni mfugaji mpangaji wa vitalu vya NARCO Kongwa kukosa huduma ya Dawa za mifugo eneo hilo jambo linalowafanya kushindwa kuhudumia mifugo yao.

Aidha, Waziri Balozi Dkt. Bashiru alisema kumekuwepo na utapeli katika suala la upatikanaji wa dawa za mifugo hivyo amelekeza huduma hiyo ipatikane katika taasisi ya wizara ikiwemo NARCO kwa upande Kongwa ili kuwaondolea adha wanauopata wafugaji kutafuta dawa za mifugo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo