DKT. BASHIRU APIGA MARUFUKU MAAMUZI YANAYOATHIRI BIASHARA ZA WAFUGAJI, WAVUVI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amepiga marufuku kwa wasimamizi wa sheria katika ngazi zote kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi kufanya maamuzi yatakayoathiri mwenendo wa biashara kwa wadau wa sekta hizo.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo Januari 15, 2025 mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa machinjio ya nyama ya Serikali iliyopo maeneo ya Kizota ambapo amewataka wasimamizi hao kuhakikisha wanaafikiana na wawekezaji na wafanyabiashara hao kwa njia ya mazungumzo.
“Haya niliyoyaona Tanga hata kama ni Halmashauri bado ni Serikali na bahati nzuri Halmashauri zote zipo chini ya Mhe. Waziri Mkuu kwa hiyo Halmashauri zote na Wizara tujizuie kufanya kazi za udhibiti kwa namna ambayo itatikisa na kuathiri shughuli za kiuchumi kwenye sekta hizi” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amewataka wataalam hao kutoa muda nyongeza kwa wafanyabishara hao na notisi ili kuwapa fursa ya kutekeleza matakwa ya sheria kabla ya kufunga bishara zao.
“Ukifunga shughuli yake kwa siku moja, watoto wake hawawezi kula na hiyo pesa hupati” Amehitimisha Balozi Dkt. Bashiru.
Kuhusiana na Machinjio ya Serikali aliyoikagua, Balozi Dkt. Bashiru amemtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambaye Machinjio hiyo ipo chini yake Bw. Mohamedi Mbwana kushughulikia dosari zote alizoziona na kuhakikisha inakuwa kwenye mazingira mazuri wakati wote.