Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

TALIRI YATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE KUONGEZA THAMANI YA MIFUGO MASOKO YA NJE YA NCHI

Imewekwa: 15 December, 2025
TALIRI YATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE KUONGEZA THAMANI YA MIFUGO MASOKO YA NJE YA NCHI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha tafiti zake zinalenga kuongeza thamani ya mazao ya Mifugo ili kukidhi masoko ya nje ya Nchi.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo aliyoifanya Desemba 15, 2025 jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ulioelekeza ufugaji wa kisasa, kibishara na wenye tija.

“Mimi niwaombe mambo matatu, la kwanza tafiti zenu zielekezwe katika kuongeza thamani ya mazao ya Mifugo na hasa katika kuuza zaidi kwenye soko la nje ili mauzo yaongezeke kutoka tani elfu 14 kwa sasa hadi tani elfu 50 ifikapo mwaka 2030” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Vilevile Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameitaka taasisi hiyo kufanya tafiti zinazohusu uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi ambapo amesisitiza ushirikiano wa kitafiti wa Taasisi za Wizara yake na ile ya Maji ili kuboresha eneo la malisho ya Mifugo na Maji.

“Jambo la tatu ni mkakati wa kuendeleza sekta ya ufugaji wa kuku kwa sababu tunataka tubadilishe sekta hiyo hapa nchini na kwenye hili tuwafate wafugaji walipo ili kutatua changamoto zao kwani wanafanya kazi kubwa hususani vijana na akina mama” Amehitimisha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Balozi Dkt. Bashiru yapo kwenye miongozo mbalimbali ya utekelezaji wa shughuli za kitafiti hivyo ameahidi yeye pamoja na timu yake kufanyia kazi maelekezo hayo.

“Yote yaliyoelekezwa ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu na tuna utaalamu hivyo tutahakikisha tunayafanyia kazi ili juhudi za Mhe. Rais Samia, malengo na Wizara na Taasisi yaweze kutimia lengo likiwa ni kuongeza kipato cha mfugaji na pato la Taifa kwa ujumla” amesema Prof. Komba.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo