​SIMIYU KUJA NA MKAKATI WA KUFIKIA MALENGO UVALISHAJI HERENI MIFUGO

Imewekwa: Monday 03, January 2022

Maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mkoa wa Simiyu na wilaya zake wametakiwa kuwa na mkakati wa pamoja kuhakikisha zoezi la uwekaji hereni za kieletrroniki kwa mifugo linafikia malengo yaliyokususdiwa.

Akizungumza hayo(21.12.2021) wakati wa utambulisho wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki Mkoani Simiyu, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Mhandisi Mashaka Luhamba amesema zoezi hilo linapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ni kati ya mikoa yenye idadi kubwa ya mifugo hapa nchini.

Mhandisi Luhamba amefafanua kuwa uongozi wa mkoa, utahakikisha unafanya ufuatiliaji na kuhitaji taarifa ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wake ili kupata matokeo chanya ya kufahamu idadi ya mifugo iliyopo Mkoani Simiyu pamoja kuiongezea thamani kwa kutoharibu ngozi za mifugo kwa kuiwekea alama kwa njia ya moto.

Akielezea juu ya mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki katika mkutano huo, Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema hereni zinawekwa kwa mnyama mwenye umri zaidi ya miezi mitatu na kwamba zitasaidia pia kupunguza muingilianio wa mifugo kutoka maeneo mengine.

Pia, amesema zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo linalofanyika kote nchini litamuwezesha mfugaji kuweza kupata mikopo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na kuikatia bima mifugo yake kwa kutumia namba za usajili zilizopo kwenye reheni ya mnyama.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mifugo Mkoa wa Simiyu Bw. Juma Kazula, akizungumza wakati wa kuahirishwa kikao hicho amesema wajumbe wamekubaliana ifikapo Tarehe 15 Mwezi Januari Mwaka 2022 kila halmashauri iwe imeandaa mpango kazi wa utekelezaji wa zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo na zoezi la uwekaji hereni likamilike Tarehe 15 Mwezi Julai Mwaka 2022 pamoja na uwepo wa taarifa ya kila mwezi juu ya zoezi hilo, huku Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Itilima Dkt. Kiraba Musoke akiwaasa wajumbe hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana ili mifugo mingi iweze kusajiliwa.

Awali maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiongozwa na Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za Mifugo wamekutana na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo kwa ajili ya kuutambulisha mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki katika mkoa huo, ambapo Bi. Kayombo amesema hereni hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza thamani ya ngozi ya mifugo ambayo imekuwa ikiharibiwa kwa kuwekewa alama kwenye ngozi kwa njia ya moto.

Zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2011 ambapo linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya Shilingi 1,750/= kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000/= kwa mbuzi na kondoo.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022