SHEMDOE APOKEA MAKASHA 70 YA KUHIFADHIA SAMAKI

Imewekwa: Saturday 31, August 2024

SHEMDOE APOKEA MAKASHA 70 YA KUHIFADHIA SAMAKI

◼️ Mkurugenzi wa Uvuvi asema mavuno Ziwa Tanganyika yamefikia zaidi ya Tani 1000 kwa siku!

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amepokea jumla ya makasha 70 ya kuhifadhia samaki kwa niaba ya wanawake wanasiriamali waliopo kwenye mialo ya Kibirizi na Katonga mkoani Kigoma yaliyotolewa na mawakala wa usafiri wa anga wa "Alliance" na Swissport leo Agosti 30, 2024 kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo mbali na kuwashukuru wadau hao wa Uvuvi Prof. Shemdoe ametoa rai kwa wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya Uvuvi kupitia nyanja mbalimbali zilizopo ndani ya uwezo wao.

"Mmeona umuhimu wa kurudisha mlichonacho kwa jamii inayotuzunguka na hii ni kwetu ni mbegu kwa sababu makasha haya yatapungumza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvuliwa na kwakuwa kushukuru ni kuomba tena nichukue fursa hii kuwaomba tena Alliance na Swissport mtushike tena mkono pale mnapoona kuna fursa ya kuwasaidia wavuvi wetu " Amesisitiza Prof. Shemdoe

Akizungumzia kiwango cha Samaki wanaovuliwa Ziwa Tanganyika kwa hivi sasa Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Prof. Mohammed Sheikh amebainisha kuwa Kiwango hicho kimefikia zaidi ya tani 1000 kwa siku kwa hivi sasa ikiwa ni taribani wiki 2 tangu shughuli za uvuvi katika Ziwa hilo zifunguliwe mkoani Kigoma.

"Kwa muda wa siku 6 za mwanzo tangu kufunguliwa kwa Ziwa Tanganyika zaidi ya tani 6,000 zimevuliwa ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ukilinganisha na tani 85,000 zilizokuwa zikivuliwa kwa mwaka mzima kabla ya kufunga Ziwa hivyo wasafirishaji mjipange vizuri kwa sababu mavuno ya mazao ya Uvuvi yataongezeka maradufu" Amesema Prof. Sheikh.

Akielezea kilichowasukuma kutoa makasha hayo kwa Wavuvi Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya usafirishaji mizigo ya Alliance Bw. Enock Mogaka amesema kuwa tukio hilo ni utekelezaji wa ombi la Waziri wa Mifugo Mhe. Abdallah Ulega alilolitoa Agosti 15, 2024 wakati wa ufunguzi wa Ziwa Tanganyika ambapo wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wavuvi katika maeneo mbalimbali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo ya Swissport Bw. Yasin Mrisho ameweka wazi kuwa wameamua kuungana kutoa makasha hayo kwa kuwa lengo la makampuni yao ni kuhakikisha Taifa linasafirisha mazao mengi zaidi ya Uvuvi nje ya nchi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Bi. Rehema Myeya amesema kuwa wanaendelea kuona matunda ya Ushirikiano baina ya Uwanja huo na wadau hao wa sekta binafsu ambapo ameahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kukuza uchumi wa nchi.

.