SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA WAFUGAJI WANAPATA MITAMBA BORA, YALENGA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZIWA
Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata mitamba bora kwa wakati kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa nchini, hatua ambayo inatokana na uchambuzi wa mradi huo, ambapo upatikanaji wa mitamba bora uliainishwa kuwa eneo linalohitaji hatua za haraka, na serikali imebainisha kuwa bado kuna haja ya kuhakikisha mitamba inawafikia wafugaji kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi leo Novemba 10, 2026 jijini Dodoma katika kikao kilichowakutanisha wadau wa sekta ya mifugo, taasisi za fedha, wamiliki wa mashamba binafsi, wasindikaji wa maziwa pamoja na taasisi za utafiti, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele amesisitiza umuhimu wa wadau hao kushirikiana kuondoa vikwazo vinavyochelewesha upatikanaji wa mitamba.
“Katika utekelezaji wa mwaka huu serikali imepanga kuanza na mitamba 405, huku mitamba 56 yenye mimba kutoka mashamba ya serikali ikitarajiwa kukabidhiwa kwa wanufaika kabla ya Desemba 15, 2026 na kupitia mradi huo, takribani Shilingi bilioni 26 zimeelekezwa TADB kwa ajili ya mtaji wa dirisha la mikopo ya mitamba, na serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 6.25 katika kuimarisha huduma za uhimilishaji, ikiwemo ununuzi wa madume bora 10 ya mbegu, mitambo tisa ya maabara, mitambo miwili ya kuzalisha hewa ya naitrojeni ya kimiminika na vifaa vya kuanzia kazi kwa wataalamu 60 wa uhimilishaji” amesema Dkt. Madele
Aidha, Dkt. Madelea amesema katika kuharakisha utekelezaji huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameelekeza wizara kuunda timu ya pamoja ya kiufundi ambayo ndani ya siku 14 itakamilisha mfumo wa viwango vya ubora wa mitamba, bei elekezi, ratiba ya upatikanaji na masharti ya mikopo, TADB kukamilisha makubaliano na benki washirika ili dirisha la mikopo lifunguliwe kabla ya mwisho wa Desemba 2026, huku TALIRI na NAIC zikitakiwa kuwasilisha ndani ya siku 30 mpango wa kuongeza uzalishaji wa mitamba bora nchini kwa kutumia teknolojia ya upandikizaji wa viinitete na mbegu zilizochaguliwa jinsia, ambapo lengo kuu ni kuhakikisha mitamba bora inawafikia wafugaji, uzalishaji wa maziwa unaongezeka na kipato cha kaya kinaboreshwa, kwa kuzingatia kugeuza wingi wa mifugo nchini kuwa tija ya kiuchumi.