​SERIKALI YATAKA USIMAMIZI MZURI ZAIDI WA SEKTA YA UVUVI, KUFIKIA MALENGO ENDELEVU

Imewekwa: Wednesday 25, January 2023

Serikali imedhamiria kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi nchini ili kuwezesha Sekta ya uvuvi kuendelea kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu ikiwa ni miongoni mwa sekta za kiuchumi zinazotoa ajira, kuimarisha usalama wa chakula, maisha ya watu pamoja na kuongeza mapato ya nje na ndani ya nchi.

Hayo yamesemwa Januari 24,2023 mjini Tanga na Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Merisia Mparazo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati ya wataalam wa mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention.

Alisema kuwa mradi huo unahakikisha kwamba kunakua na ushirikino katika usimamizi wa masuala ya Bahari na mazingira yake pamoja na rasilimali za Uvuvi zilizomo nchini.

Aidha alibainisha kuwa sekta hiyo imeajiri zaidi ya watu milioni 4.5 wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na zile zinazohusiana na uvuvi wakati takribani 194,804 ni ajira za moja kwa moja kwa wavuvi na watu 31,998 wameajiriwa katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji.

Aliongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini kwa kuhakikisha ustawi wa jamii ya wavuvi.

Alisema Serikali itaimarisha usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na kuboresha maisha ya jamii za wavuvi katika Wilaya ya Nkinga kupitia mradi wa SWIOFIC -Nairobi Convention.

"Lengo la mradi linaendana na sera ya taifa ya uvuvi ya mwaka 2015 inayoeleza kuwa rasilimali za uvuvi zinaendelezwa, zinasimamiwa, zinahifadhiwa na kutumika kwa uendelevu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya binadamu", alisema.

.