SERIKALI YAANZA KUPITIA KANUNI ZA UVUVI ZA MWAKA 2009
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kupitia Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, hatua inayolenga kuendana na mabadiliko ya kisera, kiuchumi, kimazingira na kiteknolojia yaliyotokea katika Sekta ya Uvuvi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Damas Kamani leo Agosti 31, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, aliyetaka kujua lini Serikali itapitia Kanuni za Uvuvi ili kupunguza kero zinazotokana na tozo nyingi kwa wavuvi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema mapitio hayo yamefanyika na kufanyiwa marekebisho mwaka 2026.
Mhe. Kamani amesema katika mapitio hayo, Serikali imepita upya tozo na ada mbalimbali kwa lengo la kupunguza kero na gharama kwa wavuvi na wadau wengine wa sekta hiyo, huku ikihakikisha kuwa wajibu wa Wizara wa kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za uvuvi hauathiriki.
Aidha, Serikali imeandaa na kuziunganisha Kanuni zote zinazohusu ada na tozo na kuunda Kanuni moja ya Ada na Tozo kwa Sekta ya Uvuvi. Kanuni hiyo, inayojulikana kama Kanuni za Tozo na Ada za Mwaka 2026, ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa sambamba na mchakato wa uanzishwaji wa Mamlaka ya Uvuvi.