​SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA AAT

Imewekwa: Wednesday 28, July 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewaeleza viongozi wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) kuendelea kushirikiana na serikali ili kuongeza uzalishaji wa viumbe hao.

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (27.07.2021) ofisini kwake jijini Dodoma wakati alipotembelewa na viongozi wa AAT waliokuwa na lengo la kujitambulisha na kumuelezea mpango mkakati wao wa miaka mitano pamoja na namna walivyojipanga kushirikiana na serikali katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na wizara.

Wizara inayo malengo ya kuongeza uzalishaji katika eneo la ukuzaji viumbe maji ili kuhakikisha uzalishaji huu una kuwa sawa na ule wa maji ya asili. Kwa kufanya hivi uzalishaji wa samaki hapa nchini utakuwa umeongezeka na hivyo kusaidia kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

Aidha, amewaeleza viongozi hao kuwa wizara itaendelea kushirikiana na AAT katika kazi wanayoifanya kwa kuwa malengo ya serikali ni kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi, huku akiwapongeza kwa jitihada mbalimbali ambazo tayari wameshazifanya katika kukuza uzalishaji wa viumbe maji hapa nchini.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania, Dkt. Charles Mahika amemshukuru waziri kwa utayari wake katika kuwapokea pamoja na kuwaahidi kuwapa ushirikiano katika jitihada wanazozifanya.

.