Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AHIMIZA MJADALA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI

Imewekwa: 23 December, 2025
DKT. BASHIRU AHIMIZA MJADALA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wadau wote wa sekta ya Uvuvi kushirikiana na Serikali kujadili na kupata suluhu kuhusu ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi ikiwa ni pamoja na kukomesha uvuvi usiofuata sheria na taratibu.

Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo Desemba 23,2025 wakati akizungumza na wadau wa sekta hiyo waliopo mwalo wa Kakukuru Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ambapo ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wake hatochoma nyavu za Uvuvi au kupima samaki kwa rula kama ilivyokuwa awali.

“Nimemsikia mtu wa “BMU” anataka achome haraka haraka, tunachoma kuna nini humo hata ukizichoma unapata samaki? “Amehoji Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa kama kutolindwa kwa rasilimali hizo kunaweza kusababisha mgogoro baina ya wavuvi wa dagaa dhidi ya wavuvi wa samaki na wavuvi wa Sangara dhidi ya wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba huku lawama zikielekezwa kuhamia kwa viongozi na watendaji wa Wizara.

Akizungumza kwa niaba ya Wavuvi wenzake kuhusiana na vitendo vya Uvuvi usiofaa Bw. Frank Mwijarobi amesema kuwa hatua za kukabilina na vitendo hivyo zinapaswa kuanza kuchukuliwa na wavuvi wenyewe kutokana na ukweli kuwa rasilimali watu na nyenzo za kudhibiti Uvuvi usiofuata sheria haziwiani na idadi ya watu wanaojishughulisha na vitendo hivyo.

“Mwarobaini ni sisi wenyewe wavuvi kuukataa uvuvi haramu sio viongozi wala makundi ya watu wachache kwa sababu Afisa Uvuvi ni mmoja kwenye kata na ana boti 1 ya doria lakini wavuvi haramu wapo 500 na mbaya zaidi anaishi kwenye nyumba ya mvuvi haramu, anakula kwenye hoteli za Wavuvi haramu anaweza kudhibiti vitendo hivyo?” Ameongeza Bw.Mwijarobi.

Mapema  akiwa kwenye kata ya Maliwanda Wilaya ya Bunda mkoani Mara alikofika kuzungumza na wafugaji wa eneo hilo, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndio uti wa mgongo wa uchumi na uhakika wa usalama wa chakula nchini hivyo amewataka wafugaji hao kuendelea kufuga kwa tija wakati Serikali ikiendelea kuboresha mazingira yao ya ufugaji.

Ziara ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru itaendelea Desemba 24,2025 katika mkoa wa Mwanza ambapo anatarajiwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha chakula cha samaki na kuzungumza na wavuvi wadogo waliopo mkoani humo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo