RIDHIWANI AZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amezindua Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hatua inayolenga kuimarisha mawasiliano kati ya Wizara na wadau wa sekta za mifugo na uvuvi, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Uzinduzi huo umefanyika leo Agosti 5, 2026, katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Ridhiwani amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa azma ya serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya mawasiliano, ambayo itawawezesha wafugaji, wavuvi na wadau wengine kupata taarifa sahihi na huduma kwa wakati.
Amesema kituo hicho kitasaidia kupokea maoni, maswali, ushauri na malalamiko ya wadau, pamoja na kuhakikisha changamoto zinazowasilishwa zinashughulikiwa kwa haraka kupitia wataalamu wa wizara.
"Mfumo huu utamwezesha afisa anayepokea taarifa kutoa majibu sahihi kwa wakati au kumuunganisha mdau kwa mtaalamu husika ili changamoto yake ipatiwe ufumbuzi kwa haraka," amesema Mhe. Ridhiwani.
Aidha, amesema serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha mawasiliano kati ya taasisi za umma na wananchi ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji wa huduma, na ameeleza kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuimarisha mawasiliano kati ya wataalamu wa serikali na wadau wa sekta za mifugo na uvuvi.
Mhe. Ridhiwani pia ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua hiyo, akisema ni sehemu ya jitihada za serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aidha, amewahimiza wananchi kutumia kituo hicho kuwasilisha changamoto, maoni na mapendekezo yao ili serikali iweze kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa katika sekta hizo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kunatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati na huduma bora kutoka kwa taasisi za serikali.
Amesema wizara imejipanga kuhakikisha kila changamoto inayowasilishwa kupitia kituo hicho inafanyiwa kazi kwa wakati na kwa weledi, ili kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na ucheleweshaji wa utatuzi wa changamoto.
Mhe. Kamani ameongeza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho namba yake ya Huduma ni 0737476937, ni mwanzo wa maboresho makubwa ya utoaji wa huduma, huku wizara ikiendelea kuimarisha mifumo yake ya mawasiliano kwa lengo la kuwafikia wadau wengi zaidi na kutoa huduma zenye ubora, ufanisi na kwa wakati.