Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

RIDHIWANI AONGOZA PAREDI YA MIFUGO 2026

Imewekwa: 06 August, 2026
RIDHIWANI AONGOZA PAREDI YA MIFUGO 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameongoza paredi ya Mifugo iliyofanyika Agosti 05,2026 kwenye Viwanja vya kitaifa na kimataifa vya Maonesho ya NaneNane vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa Paredi hiyo Mhe. Kikwete amesema kuwa tukio hilo linadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuimarisha sekta ya Mifugo na kuifanya kuwa moja ya nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Mifugo ni sehemu ya utamaduni, urithi na maisha yetu kwa sehemu kubwa hivyo tukio hili linaonesha fursa kwa wafugaji kuonesha mbinu na teknolojia za kisasa za utunzaji wa Mifugo” Ameongeza Mhe. Kikwete.

Aidha Mhe. Kikwete amebainisha kuwa tukio hilo linatoa fursa kwa wafugaji kujifunza kutoka kwenye ufugaji wa kujikimu na kwenda kwenye ufugaji wa kisasa unaozingatia uzalishaji wenye ubora, ubora wa bidhaa zake, ushindani wa soko na matumizi ya teknolojia” Amesisitiza Mhe. Kikwete.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amesema kuwa Mifugo yote iliyoshindanishwa kwenye paredi hiyo imetoka kwa wafugaji waliopo kwenye Halmashauri na mikoa mbalimbali nchini ambao wameamua kufanya ufugaji wa kibiashara.

“Maonesho haya pia yanatoa fursa ya kuunganisha maarifa, teknolojia na uzoefu wa wafugaji na wataalam wa huduma za ugani na kwa kufanya hivyo yanasaidia kujenga imani ya wafugaji kwa wataalam na kuwaonesha kwamba ushauri wa kitaalam una thamani na tija katika shughuli zao za kila siku” Ameongeza Mhe. Ng’wasi.

Paredi hiyo ya mwaka huu ilihusisha ng’ombe wa nyama 18, ng’ombe wa maziwa 16, mbuzi wa nyama 13, mbuzi wa maziwa 6 na mbwa 5  huku Ng’ombe aliyejulikana kwa jina la Kipara  kutoka Halmashauri ya Kondoa Mji akiibuka kinara kwa kuwa na uzito wa kilo 922.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo