Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
RASILIMALI ZA BAHARI ZATAJWA KUWA ONGEZEKO PATO LA TAIFA
RASILIMALI ZA BAHARI ZATAJWA KUWA ONGEZEKO PATO LA TAIFA
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila amesema Sekta ya Uvuvi ikisimamiwa vyema kupitia rasilimali za Bahari ya Hindi, sekta hiyo itaweza kuimarisha pato la taifa kupitia kupitia mnyororo wa thamani.
Dkt. Nguvila amesema hayo leo (19.09.2024) jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila, kwenye ufunguzi wa mkutano uliohusisha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na viongozi wa wilaya za Ilala, Kigamboni, Temeke na Kinondoni zenye maeneo yenye bahari.
Amesema kuwa mnyoyoro huo wa thamani unaohusisha wadau wa Sekta ya Uvuvi wakiwemo wavuvi wenyewe, kwenye masoko na wachakataji wa mazao ya uvuvi utakuwa na tija kwa kuhakikisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi unazingatiwa ili kupata fedha nyingi kupitia biashara ya mazao hayo.
“Samaki wanaovuliwa wakiwa wadogo kwenye soko hawaingii hivyo hauwezi kupata hesabu yao kwenye pato la taifa, hii inamaanisha ni uvuvi haramu lakini tukilinda rasimali za uvuvi vyema watavuliwa samaki wanaohitajika na pato la taifa litakuwa kubwa.” Amesema Dkt. Nguvila.
Aidha, ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya tafiti zaidi ili vizimba vya kufugia samaki viweze kutumika pia katika upande wa bahari kuu kwa kuwa yapo maeneo ambayo yanaweza kufaa kwa ajili ya uwekaji wa vizimba.
Amesema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kwa bahari kuu utasaidia kuwawezesha wadau wa Sekta ya Uvuvi kupatiwa mikopo na kufuga samaki kwa tija na kutoa fursa ya kupatiwa elimu ya ufugaji huo na kuondokana na dhana ya uvuvi haramu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi Dkt Edwin Mhede, amesema wizara imepewa mamlaka ya kuhakikisha kunakuwa na uvuvi endelevu kama moja ya mbinu ya kulinda rasilimali za uvuvi hazipotei na zinavuliwa kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo.
Dkt. Mhede amesema mkutano huo unalenga kukumbushana majukumu na umuhimu wa kuongeza ufanisi ili ulinzi wa rasilmali za uvuvi unaotakiwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uweze kutekelezwa na kwamba itaendelea kusimamia hilo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amesema lengo la mikutano ya kukutana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa ni kuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi katika maji yote ya asili zinalindwa ili kuwa na tija katika pato la taifa.
Ameongeza kuwa kumewekwa mikakati mbalimbali ya muda mrefu, mfupi na kati kwa kushirikisha wadau ili kuwa na makubaliano ya pamoja ya namna ya kulinda rasilimali za uvuvi na kuhakikisha rasilimali hizo zinazidi kuzaliana kwa wingi na kuongeza uhitaji katika masoko.
Nao baadhi ya washiriki wamesema mkutano huo umekuja muda muafaka katika kuelimishana na kuwa na mawazo ya pamoja ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinazidi kulindwa na kuwa na tija kwa taifa.