Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

QATAR YAFUNGUA SOKO LA NYAMA YA TANZANIA

Imewekwa: 18 March, 2026
QATAR YAFUNGUA SOKO LA NYAMA YA TANZANIA

Nchi ya Qatar imefungua soko la nyama ya Mbuzi na Kondoo kutoka Tanzania ambalo ililifunga Agosti 25,2025 baada ya kupata taarifa ya uwepo wa ugonjwa wa midomo na miguu (FMD).

Akizungumza mapema Machi 18,2026, Mkurugenzi wa huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amesema kuwa taarifa ya kufunguliwa soko hilo imetolewa na nchi hiyo Machi 17,2026 mara baada ya kujiridhisha kuhusu hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na magonjwa ya Mifugo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa karantini ya kisasa na awamu ya kwanza utekelezaji wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa Mifugo inayoendelea hivi sasa.

“Mara baada ya kufungiwa Serikali ilichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaandikia nchi ya Qatar kuwaeleza kuwa ugonjwa huo upo sehemu ndogo tu ya nchi yetu na mifugo tunayopeleka huko haitoki kwenye maeneo hayo na bahati nzuri machinjio zetu zote hapa nchini zina sifa ya kuchakata nyama inayokwenda nje hivyo na wao baada ya kujiridhisha ndo wakatufungulia” Ameongeza Dkt. Lutege.

Aidha Dkt. Lutege amebainisha kuwa soko hilo limefunguliwa kwa sharti la kila mzigo wa nyama unaotaka kupelekwa kwenye nchi hiyo kupimwa na kuthibitishwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) ambayo imeonekana kuwa na sifa stahiki ya kufanya kazi hiyo.

Kufunguliwa kwa soko hilo kunatarajia kuongeza kiwango cha mauzo ya nyama nje ya nchi ambapo awali nchi hiyo ilikuwa ikipokea takribani tani 3000 kutoka Tanzania.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo