BUNGE LAPONGEZA MAFANIKIO YA CHANJO NA UTAMBUZI WA MIFUGO
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kamati yake ya kudumu Viwanda, Biashara, Kilimo limepongeza mafanikio yaliyotokana na kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchini iliyoanza miezi kadhaa iliyopita.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 16,2026 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika wakati wa ziara ya kamati yake Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro walikofika kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa kampeni hiyo ambapo ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa usimamizi mzuri wa kampeni hiyo kuanzia ngazi ya elimu kwa wafugaji.
“Kwa kipindi hiki cha miezi michache ambayo kazi hii imeanza tayari nchi yetu imefungua baadhi ya masoko na imesafisha jina lake kuwa ni moja ya nchi zilizoingia kwenye mpango mkubwa wa chanjo hivyo sisi tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya 6 lakini kwa namna ya pekee tunaipongeza sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi” Ameongeza Mhe. Mwanyika.
Aidha Mhe. Mwanyika amesifu jitihada zilizofanywa na Wizara kwa kulihakikishia Bunge mafanikio ya utekelezaji wa kampeni hiyo kupitia ushawishi walioufanya kutokana na elimu waliyoisambaza kwa wafugaji hali iliyosababisha kuongezeka kwa wito wa wafugaji kwenye zoezi hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekipongeza Chama cha wafugaji nchini kwa namna walivyounga mkono jitihada za Serikali kwenye utekelezaji wa zoezi hilo ambapo amekiri isingekuwa rahisi kama wasingefanya hivyo.
“Kwa muda mrefu nchi yetu haijawahi kufanya chanjo ya jumla kwa nchi nzima na jambo hili lilikuwa na upotoshaji mwingi kuhusu ubora wa chanjo, hereni huku wengine wakifanya mizaha kuwa ng’ombe wanavalishwa hereni kama binadamu lakini Chama cha wafugaji kilisimama na kutoa ufafanuzi wa kitaalamu faida na umuhimu wa chanjo na kutambua mifugo” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha wafugaji nchini Katibu wa Chama hicho Bw. Mathayo Daniel amesema kuwa wamelipokea na kutekeleza zoezi hilo baada ya kutambua faida watakazopata baada ya mifugo yao kuchanjwa na kutambuliwa.
“Chanjo hii sisi wafugaji imetuokoa sana pamoja na uwepo wa msimu mrefu wa kiangazi hakuna mfugaji aliyeua mifugo yake kwa ugonjwa wa mapafu hivyo tunaiomba Serikali itutafutie pia chanjo ya ugonjwa wa midomo na miguu” Ameongeza Bw. Daniel.
Kamati hiyo ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imehitimisha ziara yake kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi ambapo ilianza kwa kutembelea Shirika la Uvuvi nchini TAFICO Machi 13,2026 jijini Dar-es-salaam.