MATUNDA BBT-UVUVI AWAMU YA PILI YAANZA KUONEKANA
Utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa upande wa sekta ya Uvuvi umeanza kuonesha matunda baada ya samaki waliopandikizwa takribani miezi 3 iliyopita kuanza kukua hadi kufikia gramu 250
Akizungumza mmoja wa wanufaika hao Bw. Erasto Deo mbali na kuishukuru Serikali kwa kuwawezesha mikopo ya masharti nafuu isiyo na riba amesema kuwa hatua hiyo imewaonesha mwanga wa mafanikio wanayotarajia pindi watakapovuna samaki hao kuanzia mwezi Novemba mwaka huu.
“Mikopo hii ina manufaa makubwa sana kwa sababu kwa mfano sisi tulipandikiza vifaranga 11,000 ambavyo kama vitaendelea kukua vizuri hadi kufikia gramu 500 tuna uhakika wa kupata tani tano na nusu ambapo kwa bei ya sasa ya kilo ya samaki hapa Mwanza bei ya huku uwandani ni shilingi 8500 hivyo hata tukipata tani 4 tuna uhakika wa kupata milioni 32 ambayo kiuhalisia mtu akikopa hela hiyo atarudisha milioni 60 kwa miaka 5” Ameongeza Bw. Deo.
Kwa upande wake mratibu wa programu hiyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Clemence Katunzi amesema kuwa matokeo hayo yanatokana na kujitoa kwa vijana hao kwenye huduma mbalimbali za ufugaji wa samaki hao.
Naye mratibu wa programu hiyo kutoka Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Bw. Mashaka Kapagalla amesema kuwa Taasisi yake inatekeleza majukumu mbalimbali katika kufanikisha programu hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapa ujuzi wa mara kwa mara kuanzia siku ambayo vijana hao wanapandikiza vifaranga kwenye vizimba.
“Lakini jukumu la pili kupitia mitaji yao FETA ina jukumu la kutoa zile pembejeo ikiwemo vifaranga vya samaki, vyakula na vitu vingine vinavyohusiana na uzalishaji” Amesema Bw. Kapagalla.
Awamu ya pili ya utoaji wa mitaji kupitia programu ya Jenga kesho iliyo bora inatarajiwa kuendelea kwenye Wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo takribani vijana 85 wanatarajia kunufaika na programu hiyo.