MWONGOZO MPYA KUWASAIDIA WAVUVI MAJI MADOGO NA MAENEO OEVU

Imewekwa: Thursday 04, July 2024

MWONGOZO MPYA KUWASAIDIA WAVUVI MAJI MADOGO NA MAENEO OEVU

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uvuvi kwenye Maji madogo ikiwa ni njia mojawapo ya kuweka usimamizi mathubuti kulingana na changamoto ambazo zipo kwenye haya maeneo ili wavuvi waweze fanya shughuli za uvuvi kirahisi kutokana na sehemu waliopo na nyakati zilizopo.

Akizungumza, leo Juni 28, 2024 mkoani Dodoma katika kikao cha wadau kupitia Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema Wizara imeamua kuandaa muongozo huu na kuupa kipaumbele kwa lengo la kusaidia wavuvi na taifa kupitia sekta ya uvuvi ili nchi iendelee kushamiri katika uzalishaji wa zao la uvuvi.

"kanuni ya 58b ya kanuni za uvuvi za toleo la 2020, ilitutaka kuandaa Muongozo utakaosaidia kuratibu, kufafanua na kuongoza shughuli hizi zinazoambatana na uvuvi wa kwenye maji madogo na maeneo oevu", amesema Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede alisema lengo kubwa la kuunda muongozo huu ni kuboresha muktza mzima wa usimamizi wa shughuli za uvuvi na uvunaji wa rasilimali za uvuvi na mazao yake zinazopatikana katika maji madogo lakini pia na kwenye maeneo oevu na sehemu mbalimbali za taifa letu, na kwa hili serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya uvuvi ikiwa ni kwa wale waliomo ndani ya nchi na nje ya nchi katika kuhakikisha kwamba uvuvi unaofanyika unakuwa endelevu katika maji madogo na maeneo oevu ili kuongeza pato la wavuvi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Bugomba Kimasa amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina dhamana ya kusimamia rasilimali za uvuvi nchini na ndio mana inakuwa na ulazima wakuwa na chombo ambacho kitasaidia katika kusimamia rasilimali za uvuvi kwenye maeneo mbalimbali.

Vilevile Bw. Kimasa amesema Wizara imeandaa muongozo wa usimamizi wa uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu ambao utaweka usimamizi mathubuti katika maeneo hayo kwa sababu maeneo haya ni muhimu.

"Tumeandaa Rasimu ya huu muongozo kwa lengo la kutusaidia kuweza kuwa na usimamizi mathubuti kulingana na changamoto ambazo zipo kwenye haya maeneo kwa sababu maeneo mengine yanapata maji kwa msimu na mengine yanapata maji kwa mwaka mzima, sasa na sisi Sheria zetu za uvuvi zimeweka ukomo wa macho ya nyavu ambayo yanatakiwa kuvua katika yale maeneo, sasa ikifikia maji yamekauka wale samaki wanatakiwa kuvunwa lakini zile nyavu zilizopendekezwa kwa mujibu wa Sheria haiwezi kuwavua, kwa hiyo inabidi sasa tuwe na chombo kitakachosimamia katika maeneo haya." amesema Bw. Kimasa

Akitoa ufafanuzi juu ya sheria ya Uvuvi, Afisa Uvuvi Wilaya ya Karatu, Bw. Frank Elisante amesema, sheria iliyopo inasema kwamba samaki wanatakiwa wavuliwe kwa kutumia nyavu ya inchi 3, lakini kuna kipindi maji ukauka kwenye mito kiasi cha kwamba samaki hawapatikani kabisa, kwa hiyo kwa muongozo huu utaenda kufanya mabadiriko kiasi cha kwamba wale samaki ambao watakuwa wanapatikana kipindi cha kihangazi ambao hawafiki inchi 3, wataweza kuvuliwa bila shida yeyote na mahali popote.

Bw. Elisante aliendelea kusema kuwa huu utakuwa muongozo mzuri ambao utakuwa na matokeo chanya kwa serikali pamoja na wavuvi, japo kuna changamoto kadhaa, ikiwemo uvuvi wa samaki wadogo ambao ni kinyume cha sheria.

Naye, Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Bi. Devotha Gachuni amesema, maeneo mengi ya wilaya ya Kaliua ni

ardhi oevu yanayotokana na Mto Ugala na Sagala, na pia kuna maji endelevu na shughuli za uvuvi zinaendelea.

Pia Bi. Devotha ameongezea kuwa muongozo huu wa Usimamizi wa uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu utawafanya wavuvi waendelee kuvua kwa tija na samaki kukua vizuri pamoja na kuongezea kwa wingi, japo kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uvuvi haramu unaoendelea mpaka sasa.

.