​MNYETI ATANGAZA KIAMA CHA WAVUVI HARAMU ZIWA TANGANYIKA

Imewekwa: Monday 20, November 2023

MNYETI ATANGAZA KIAMA CHA WAVUVI HARAMU ZIWA TANGANYIKA

Ni wakati wa hafla ya kugawa boti wilayani Kalambo

Kufuatia malalamiko ya Wavuvi wa Wilaya ya Kalambo kuhusu vitendo vya uvuvi haramu vinavyofanywa na wavuvi wanaodaiwa kutoka nchi jirani ya Zambia hali itakayowakwamisha kupata samaki wa kutosha hata wakiwa na vifaa vya kisasa, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ametangaza vita kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo katika Ziwa Tanganyika ambapo ameweka wazi mipango ya Serikali kupitia Wizara yake kuunda kikosi kazi maalum kitakachoshughulikia jambo hilo.

Mhe. Mnyeti amesema hayo wakati wa hafla ya kugawa boti 2 za Uvuvi kwenye bandari ndogo ya Kalambo mkoani Rukwa ambapo amesisitiza kuwa rasilimali za Uvuvi zinazopatikana upande wa Tanzania ni lazima zilindwe dhidi ya wale wote wanaozichukua kinyume na utaratibu na sheria.

“Tunawapenda na tunawakaribisha sana wageni kutoka nchi jirani lakini ni lazima wafuate taratibu na sheria za nchi yetu na taarifa tulizonazo hapa ni kwamba wageni hawa wanashirikiana na maafisa uvuvi wa maeneo haya na nitoe onyo kwa wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivi tutawashughulikia” Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Mhe. Mnyeti ameitaka kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kalambo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Lazaro Komba kuanza kuchukua hatua za awali kudhibiti vitendo hivyo na kukipa ushirikiano kikosi kazi kitakachoundwa na Wizara ili vitendo hivyo viweze kukomeshwa.

“Hii ni rasilimali iliyopo upande wa Tanzania na inapaswa kuwanufaisha Watanzania kwa sababu hata huko Zambia wananufaika na rasilimali hii kwa upande wao na ninasikia hawa wavuvi haramu wamekimbilia huku kwetu baada ya nchi yao kuwadhibiti kule hivyo nasi hatutaruhusu hilo” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Lazaro Komba mbali na kuahidi kushughulikia changamoto hiyo ya Uvuvi haramu Wilayani kwake amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wavuvi wa Wilaya hiyo wanakuwa ni miongoni mwa wanufaika wa mkopo usio na riba wa boti za Uvuvi ambapo ameahidi kuwasimamia wanufaika hao ili waweze kuzitumia katika matumizi stahiki.

Akizungumza kwa niaba ya wavuvi wenzake walionufanika na mkopo huo, Mwenyekiti wa chama cha Wavuvi mkoani Rukwa (RUFIMA) Bw.Peter Mpangala ameishukuru Serikali kwa kuwapatia boti hizo ambazo amebainisha kuwa zitapunguza na kuondoa changamoto ya uvuaji wa samaki wa kutosha iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

.