​MIFUGO ZAIDI YA MILIONI 370 IMEPATIWA CHANJO DHIDI YA MAGONJWA

Imewekwa: Tuesday 08, April 2025

Na. Chiku Makwai

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa chanjo kwa mifugo zaidi ya milioni 370 kwa lengo la kutibu na kuzuia magonjwa aina ya kiimeta na homa ya mapafu, pamoja na mifugo kukidhi matakwa ya soko la kimataifa.

Hayo yameelezwa leo (Aprili 9, 2025) na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akitoa hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio na Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma.

“Kwa kuimarisha huduma za ugani na kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mipaka, katika kipindi cha Mwezi Julai, 2024 hadi Mwezi Januari 2025, serikali imenunua chanjo zenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.1 kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchin.i” amesema Mhe. Waziri Mkuu

Aidha Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa kisasa unaozingatia malisho bora na idadi ya mifugo inayoweza kuleta tija kwa mfugaji serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo ambapo ujenzi wa mabwawa manne ya Bukabwa (Butiama), Kihumbu (Bunda), Isulamilomo (Nsimbo) na Kwenkikwembe (Kilindi).

Ameongeza kuwa kutokana na Kampeni ya Tutunzane Mvomero iliyozinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uzalishaji wa mbegu za malisho umeongezeka kutoka tani 127.8 Mwaka 2023/2024 hadi tani 152.67 Mwaka 2024/2025 na uzalishaji wa malisho yaliyosindikwa umeongezeka kutoka tani 728.6 hadi tani 2,669.84.

Aidha, amesema kuwa kutokana na jitahada zilizofanyika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2024/2025 uzalishaji wa mifugo umeongezeka na kufikia milioni 189.8 kutoka mifugo milioni 181.8 Mwaka 2023/2024, Ongezeko hilo limechangia uzalishaji wa nyama kutoka tani 963,856.55 kwa Mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 1,054,114.03 Mwezi Februari, 2025.

Pia, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na huduma za chanjo ya mifugo, kujenga na kukarabati minada ya mifugo, kujenga machinjio ya kisasa na kuimarisha mashamba darasa ya malisho.

Kwa Upande wa Sekta Ya Uvuvi Mhe Waziri Mkuu amesema kuwa serikali imeendelea kutekeleza mradi wa mikopo nafuu kwa wananchi ili kuwekeza katika ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambapo mikopo ya Shilingi Bilioni 36.64 imetolewa kwa wanufaika 7,130. Kupitia mikopo hiyo, ajira 3,000 za moja kwa moja, na zaidi ya 1,000 katika mnyororo wa thamani zimezalishwa.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa-Masoko na ujenzi huo utahusisha gati lenye urefu wa mita za mraba 315, jengo la utawala na vyumba baridi vya kuhifadhia samaki kwa gharama ya Shilingi Bilioni 289.5 umefikia asilimia 79 na ujenzi utakapokamilika unakadiriwa kuhudumia tani 60,000 za mazao ya uvuvi kwa mwaka na kutoa fursa za ajira takriban 30,000.

Mwisho Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 serikali itaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko mkoani Lindi pia kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kuimarisha huduma za utafiti, mafunzo na ugani.

.