SERIKALI YAHAMASISHA MATUMIZI YA MAYAI, MAZIWA TANGA

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wake wa Tasnia ya Maziwa na Kuku imeendesha kampeni ya kuhamasisha ulaji wa mayai na unywaji wa maziwa kupitia zoezi la ugawaji wa mazao hayo ya Mifugo kwenye shule za watoto wenye mahitaji maalum lililofanyika Oktoba 13,2025 jijini Tanga.
Akizungumza wakati wa uendeshaji kampeni hiyo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Mary Yongolo amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuinua kiwango cha ulaji wa mazao hayo kwa kujenga utamaduni wa matumizi yake kwa watoto hususan wanafunzi ili kujenga nguvu kazi ya Taifa itakayokuwa imara na yenye afya.
“Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inasema Tuungane pamoja kupata lishe bora kwa maisha ya sasa na ya baadaye na maisha ya baadae yanaanza utotoni kwa makundi haya madogo tuliyokuja kuyatembelea hapa” Ameongeza Bi. Yongolo.
Akizungumzia umuhimu wa mayai na maziwa kwa wanafunzi, Afisa Lishe wa mkoa huo Bi. Sakina Mustapha amesema kuwa maziwa yana protini inayosaidia kujenga mwili huku pia akiongezea kuwa zao hilo lina asili ya maji yanayomfanya mnywaji kukidhi kiu yake
“Kwenye maziwa pia kuna madini mbalimbali yanayosaidia kuimarisha mifupa lakini kwa upande wa mayai mbali na kuwa na vitamini na madini mbalimbali kuna mafuta ya asili kupitia kiini chake na vyote hivyo vinasaidia kujenga mwili hususani katika makuzi ya ubongo kwa mtoto” Ameongeza Bi. Mustapha.
Kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mazao mbalimbali ya Mifugo na Uvuvi hufanyika kila mwaka wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa lengo la kuinua kiwango cha ulaji wa mazao hayo yanayotajwa kuchangia sehemu kubwa ya protini kwenye mwili wa binadamu.