Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KAMANI AHITIMISHA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI 350 WA SEKTA YA UVUVI

Imewekwa: 12 January, 2026
MHE. KAMANI AHITIMISHA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI 350 WA SEKTA YA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani amewataka wajasiriamali 350 wa sekta ya uvuvi waliopata mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi  kutumia ujuzi walioupata kwa ajili ya kuongeza ajira, Kipato na kuchagia  Maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa kufunga  Mafunzo hayo  Leo Januari 9, 2026 katika Ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi Mhe. Kamani amesema serikali inaendelea kuunga Mkono wajasiriamali wanaojihusisha na uongezaji wa thamani ya mazao ya uvuvi ili kupanua biashara zao.

"Mafunzo hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake na vijana, kupitia fursa za Uchumi wa Buluu, leo mnapopewa vyeti mnakabidhiwa dhima ya kwenda kutumia ujuzi wenu kuongeza ajira, kipato na maendeleo ya Taifa"  alisema Mhe. Kamani.

Aidha, aliongeza kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Wakala ya  Elimu na Mafunzo ya Uvuvi  ili kuongeza ufanisi unaolenga kutoa mafunzo bora ya kukuza sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu 

Kwa Upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na  Shirika la Maendeleo la Ubelgiji la ENABEL kupitia mradi wa Green and Smart Cities (IncluCities) yamelenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, ushindani wa bidhaa sokoni na kuongeza kipato cha kaya.

 Awali wawakilishi wa Kundi la Vijana na Kina Mama Wajasiriliamali wakiwasilisha risala yao kwa mgeni rasmi  walieleza kuwa mafunzo hayo yataenda kubadilisha mfumo mzima wa uchakataji  na uongezaji wa thamani wa mazao ya Uvuvi tofauti na hapo awali walipokuwa wakitumia njia za jadi.

Jumla ya kina mama wajasiriamali 200 wamehitimu mafunzo ya usindikaji wa mazao ya samaki, huku vijana 150 wakipata mafunzo ya utayari kazini katika ukuzaji viumbe maji.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo