Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

BUNGE LAPITISHWA MRADI WA MAGEUZI TASNIA YA MAZIWA, MABADILIKO YA TABIANCHI

Imewekwa: 05 November, 2026
BUNGE LAPITISHWA MRADI WA MAGEUZI TASNIA YA MAZIWA, MABADILIKO YA TABIANCHI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani ameiongoza Wizara yake kulipitisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi kwenye semina fupi iliyofanyika Novemba 05,2026 Bungeni jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kujengewa uelewa kuhusu mradi huo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Mariam Ditopite ametoa wito kwa wabunge kuwa mabalozi wa mradi huo kwenye maeneo yao unakotekelezwa ili kusaidia wafugaji kubadilika na kurasimisha biashara ya maziwa nchini.

“Tumeona mfumo mzima wa uuzaji wa maziwa yetu mengi yanaenda kwenye masoko yasiyo rasmi hivyo kwa utaratibu huu wa kujenga vituo vya kukusanyia maziwa na vifaa vya kisasa vya kusambazia maziwa naamini tutakuwa tumetibu changamoto hiyo” Amesema Mhe. Ditopile

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani mbali na kulishukuru Bunge kwa kuwapa fursa ya kuwapitisha kwenye mradi huo ameahidi kufanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wabunge hao.

“Tunakwenda kukaa chini kuangalia muundo wa mradi wetu hasa kwenye sehemu ya maeneo ambayo ndo imekuwa ishu kubwa tuone namna ya kuweka ili manufaa yaweze kusambaa kwa upana unaostahili na maoni mliyotoa leo sio tu yatatusaidia kwenye awamu hii bali pia yatatusaidia kuboresha awamu zote zinazofuata” Amesema Mhe. Kamani.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya mradi huo,  Mratibu wa Mradi huo Dkt. Lazaro Kapella amesema kuwa mradi huo unalenga kuwaondoa wafugaji kwenye ufugaji wa mazoea na kuwafanya wafuge kibishara huku pia ukiongeza usalama wa maziwa yanayozalishwa.

“Kwa bajeti ya mwaka huu wa kwanza mradi huu una thamani ya takribani shilingi Bil.110 ambayo imegawanywa katika maeneo matatu ambapo eneo la Uzalishaji linatarajiwa kutumia Dola milioni 19, uchakataji na unywaji maziwa vikitarajiwa kutumia Dola milioni 17.5 huku upande wa usimamizi na uratibu ukitarajiwa kutumia Dola Mil.5.3” Amesema Dkt. Kapella.

Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi unatekelezwa katika mikoa nane nchini ambayo ni Arusha, Iringa, Mbeya,Njombe,Tanga, Morogoro, Pwani na Kilimanjaro.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo