Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa-Kazi na Utu, Tunasonga Mbele, Kazi na Tabasamu, Tunasonga Mbele.

Imewekwa: 15 December, 2025
Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa-Kazi na Utu, Tunasonga Mbele, Kazi na Tabasamu, Tunasonga Mbele.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amezindua rasmi salaam ya wizara hiyo na nembo yake yenye usemi "Kazi na Utu, Tunasonga Mbele, Kazi na Tabasamu, Tunasonga Mbele" ili kuunga mkono maono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta tabasamu kwa wananchi. 

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amebainisha hayo leo (15.12.2025) jijini Dodoma, kwenye kikao kazi na watumishi wa wizara hiyo, kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, ambapo amesema wakati akifungua Bunge la 13 Mhe. Rais Dkt. Samia alisema anamuomba Mwenyezi MUNGU kuwa mwisho wa utumishi wa serikali ya awamu ya sita usipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa bali tabasamu kwa watanzania.

Ameongeza kuwa sekta za mifugo na uvuvi ni miongoni mwa sekta ambazo zikifanya vizuri Mhe. Rais ataacha kumbukumbu hususan tabasamu la utu kwenye nyuso za watanzania. 

Aidha, amesema masuala mbalimbali ambayo yanapaswa kufanyika katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi yanafuata msingi wa maono ya Mhe. Rais ya 4R kwenye mageuzi, ustahimilivu, maridhiano na kujenga upya. 

Katika kuzingatia hayo, amewataka watumishi kuzingatia utawala wa sheria, nidhamu na umakini wa kuamua, kusema na kutenda kwa kila hatua. 

Pia, amewakumbusha watumishi kufanya kazi kama timu moja na kufuata utaratibu wa kazi, ambapo kila mtumishi ajisikie yuko sawa kwa kuwa kila mmoja ana umuhimu katika majukumu yake.

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amefafanua pia umuhimu wa kuwajibika kwa umma kwa watumishi na kueleza yote yanayofanywa na yanayopangwa kufanywa, kuelezwa kwa kina katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Amewakumbusha pia watumishi kuwa tayari kusikia yanayosemwa juu ya wizara na kuwepo kwa mfumo mzuri wa ufuatiliaji ili kurekebisha na kuyafanyia kazi maoni ya wananchi. 

Amekitaka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kufanya kazi katika majira ya sasa na kufafanua jambo lolote linalohitaji ufafanuzi kwa umma, kadri inavyowezekana. 

Katika hatua nyingine amewapongeza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mapokezi mazuri ambayo imekuwa ishara ya kuwapatia nguvu kutimiza majukumu yao pamoja na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani. 

Kwa upande wake Mhe. Naibu Waziri Kamani, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake aliyoweka kwake kuhudumu katika wizara hiyo, kwa kuwa ni sekta muhimu katika kuchochea kutoa ajira na lishe. 

Ameongeza kuwa amekuta kazi kubwa imefanyika kwa ushirikiano mkubwa wa watumishi na kwamba sekta za mifugo na uvuvi ni muhimu katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa. 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena, amesema wizara hiyo ina watumishi 1,042 wanaotekeleza majukumu kwenye vituo mbalimbali. 

Amesema katika kupunguza makali ya hali ya kifedha ya watumishi hao, wizara inafanya utaratibu wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili iwe sehemu ya watumishi kunufaika na mfuko huo kifedha.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amesema kila kinachofanywa na wizara ni kuhakikisha watu wananufaika kiuchumi na kijamii hususan kwa lishe katika sekta za mifugo na uvuvi. 

Amebainisha kuwa protini inayopatikana kwa wanyama na mazao ya uvuvi ni muhimu katika mwili wa binadamu kwenye makuzi yake. 

Katika kikao kazi hicho cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na watumishi wa wizara kwenye makao makuu ya ofisi hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, baadhi ya wafanyakazi walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao katika kukuza sekta hizo na kuboreshwa mazingira ya watumishi katika kutekeleza majukumu yao.
 

Mrejesho, Malalamiko au Wazo