​KIWANDA CHA UTAMBUZI WA MIFUGO KWA KUTUMIA HERENI CHAZINDULIWA

Imewekwa: Tuesday 28, September 2021

Serikali imesema matumizi ya mfumo wa kisasa wa kuvisha mifugo hereni za kieletroniki katika usajili, utambuzi na kuweka alama utasaidia kupunguza changamoto za wizi wa mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, ameeleza hayo jana (06.09.2021) wakati akizindua kiwanda cha kutengeneza hereni za mifugo cha Kampuni ya S & J Animal Tech Ltd kilichopo jijini Dar es Salaam, ambapo inatajwa mfumo huo utakuwa wa kisasa zaidi katika kuweka alama za mifugo mbalimbali ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.

“Mifugo hiyo, ilikuwa ikiwekwa alama, utambuzi na kusajiliwa kwa njia kupiga chapa kwa kutumia chuma maalumu kinachowekwa katika moto kisha kuwekwa kwenye ngozi ya mbuzi, ng’ombe au kondoo kwa ajili ya alama. Njia hiyo ililamikiwa na baadhi ya wafugaji waliodai mifugo yao hasa ng’ombe inaharibika hususan ngozi. Lakini mfumo wa hereni anayovishwa mfugo kweny sikio inatajwa kuwa bora zaidi tofauti na mfumo wa awali.” Amesema Mhe. Ndaki

Ameongeza kuwa suala la matumizi ya mfumo wa hereni katika mifugo ni la msingi huku akiwataka viongozi wa chama cha wafugaji waliowakilisha wenzao katika uzinduzi huo, kwenda kutoa elimu kuhusu teknolojia hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo, Prof. Hezron Nonga amesema mfumo huo ni njia bora isiyoleta madhara kwa mifugo, na pia itahifadhi taarifa na hereni hizo zimetengenezwa kwa malighafi bora zaidi.

Prof. Nonga amesema hereni hizo zitakuwa na namba maalum ya Tanzania, namba ya mkoa na wilaya pamoja na namba za mifugo. Pia ndani katika hereni hiyo kuna alama yenye uwezo wa kuhifadhi taarifa zote na kuzituma katika mtandao.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Shannel Ngowi amesema utambuzi kwa kutumia mfumo wa hereni umeshaanza na tayari mifugo 200,000 imeshavalishwa hadi kufikia tarehe 05 Mwezi Septemba mwaka huu huku akibainisha kuwa zaidi ya ng’ombe 70,000 wameshatambuliwa katika wilaya za Kalambo na Nkasi mkoani Rukwa.

.