KAMANI AFUNGA BUNGE LA VIJANA, AWATAKA VIJANA KUWA VIONGOZI WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA TAIFA
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani (MB), leo Novemba 13, 2026 amefunga rasmi Bunge la Vijana la mwaka 2026 katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni, Dodoma, akiwataka vijana nchini kutumia elimu, maarifa na uzoefu walioupata kupitia jukwaa hilo kuwa chachu ya uongozi bora na maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kamani amesema Bunge la Vijana ni jukwaa muhimu la kukuza uelewa wa mfumo wa kibunge, kujenga uwezo wa uongozi, kuimarisha misingi ya demokrasia na kuwawezesha vijana kujieleza, kujenga hoja na kufanya maamuzi kwa kuzingatia maridhiano na maslahi mapana ya umma, na ameeleza kuwa ushiriki wa vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Bunge na Serikali wakati wa mkutano huo umewapa uzoefu muhimu wa kiuongozi.
Aidha, Mhe. Kamani amewapongeza wabunge wote wa Bunge la Vijana kwa ushiriki wao, akisisitiza kuwa mchango wa kila mbunge ni muhimu katika kutekeleza majukumu ya kibunge, ikiwemo kujadili masuala ya kitaifa, kuchambua miswada, bajeti na kuisimamia Serikali, na amesema kuwa vijana wanapaswa kuwa watu wanaotoa suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii badala ya kuwa walalamikaji.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge kupitia kaulimbiu ya “Miaka 100 ya Bunge, Historia Yetu, Dira Yetu,” Mheshimiwa Kamani amewataka vijana kujifunza na kuienzi historia ya Bunge ili kuitumia kama msingi wa kujenga Bunge bora kwa vizazi vijavyo, na ameiomba Ofisi ya Bunge kuendeleza mawazo yaliyotolewa na Bunge la Vijana kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za kihistoria, kuanzishwa kwa kituo cha urithi wa masuala ya kibunge na kujengwa kwa mnara wa miaka 100 ya Bunge.
Vilevile, Mhe. Kamani amewahimiza washiriki kutumia mafunzo waliyoyapata katika vyuo vyao na kuyashirikisha kwa vijana wengine, akieleza kuwa Taifa linahitaji viongozi vijana wenye uzalendo, uadilifu, uchapakazi na mtazamo chanya, na ameipongeza Ofisi ya Bunge kwa kuanzisha na kuendeleza programu hiyo, huku akibainisha kuwa Bunge la Vijana ni jukwaa endelevu litakalofanyika kila mwaka. Mwishoni mwa hotuba yake, ametamka rasmi kufungwa kwa Bunge la Vijana la mwaka 2026.
Kwa upande wake, Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (Mrembo) amesema jukwaa la Bunge la vijana ni Jukwaa rasmi ambalo lina lengo la kuwapa vijana nafasi ya kushiriki katika mijadala ya masuala ya Kitaifa, kutoa maoni na kujifunza taratibu za kibunge, kidemokrasia pamoja na kushiriki katika kutoa mapendekezo kuhusu sera, Sheria na Mipango ya Maendeleo inayowahisu vijana wenyewe.
Naye, Spika wa Bunge la Vijana la mwaka 2026, Mhe. Anna Denis Mrema amesema kupitia Bunge hilo wamejifunza mengi, ikiwemo historia ya Bunge, taratibu za uendeshaji wa Bunge, nidhamu ya uongozi ambayo itaenda kuleta tija katika Maendeleo ya Taifa.