Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
HERENI ZA KIELEKTRONIKI KUKUZA THAMANI YA SOKO LA MIFUGO NA MAZAO YAKE

Matumizi ya hereni za kielektroniki kwenye utambuzi wa mifugo yatasaidia kuongeza thamani katika soko la mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Haya yamesemwa leo (22.12.2021) na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba wakati akifungua mkutano wa uhamasishaji utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa Mgumba amesema kuwa wanunuzi wa mifugo na mazao yake hasa kutoka nje ya nchi wamekuwa wakihitaji kupata taarifa za mifugo kwa lengo la kujua ubora wake. Na tayari Rais Samia Hassan ameshatafuta masoko ya mifugo na mazao yake nje ya nchi, hivyo utambuzi huo wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki umekuja muda muafaka kwani utakwenda kusaidia kupatikana kwa taarifa za mifugo kwa usahihi na kwa wakati.
Vilevile amewasihi wafugaji na wadau wengine wa mifugo kuendelea kuhamasishana juu ya matumizi ya hereni hizo ambazo kwa ng’ombe na punda zinawekwa kwa shilingi 1,750 kwa mfugo na kwa mbuzi na kondoo zinawekwa kwa shilingi 1,000 kwa mfugo.
Mkuu wa Mkoa Mgumba amewaeleza washiriki wa mkutano kuwa wanatakiwa kuelimisha na kuwahamasisha wafugaji juu ya umuhimu wa matumizi ya hereni hizo ambazo zitasaidia katika kupata trakwimu halisi ya mifugo iliyopo katika eneo husika, kudhibiti wizi wa mifugo, kuongeza thamani ya mifugo pamoja na mazao yake.
Vilevile amewaagiza viongozi wa vijiji kuhakikisha wanaweka mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao ili eneo kwa ajili ya wafugaji liweze kujulikana na kukabidhiwa kwa wafugaji ambao wapo tayari kulitumia kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kuondoa migogoro iliyopo ya mfugaji na mtumiaji mwingine wa ardhi.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Songwe pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanalisimamia zoezi hili kwa umakini mkubwa. Pia amewataka watambue kuwa zoezi hilo ni kwa lengo la kuwasaidia wafugaji na sio biashara hivyo hatarajii kutokea mkwamo wa aina yoyote.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa utambuzi huu wa kutumia hereni za mifugo ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya mifugo kwa kuwa unakwenda kuongeza thamani ya mifugo na mazao yake.
Lakini pia utaratibu uliokuwa ukitumika wa kuwatambua mifugo kwa kutumia chapa za moto ulikuwa unakiuka haki za wanyama kwani Wanyama walikuwa wakipata maumifu makali ambapo wengine kutokana na kupigwa chapa vibaya iliwasababishia kufa. Utambuzi huu wa kutumia hereni za kielektroniki unawezesha taarifa zote muhimu za mfugo kupatikana kuanzia akiwa mdogo mpaka anapoingia sokoni hivyo ni rahisi kwa mtu aliyepo nje ya nchi kupata taarifa endapo atazihitaji akiwa huko huko.
Prof. Nonga amewaeleza washiriki hao wa mkutano kuwa utekelezaji wa zoezi hili la utambuzi kwa kutumia hereni za kielektroniki unaweza kufanyika kwa kutumia vijana waliopo katika vijiji kitu ambacho kitasaidia sana katika kupunguza gharama ya uwekaji wa hereni hizo kwenye mifugo.
Julius Nyingi ambaye aliwawakilisha wafugaji kutoka wilaya ya Mbozi amesema kuwa utaratibu wa utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki utawasaidia sana wafugaji kwani utawezesha kujulikana kwa idadi ya mifugo katika eneo na hivyo kusaidia kwenye uwekaji wa mipango ya maendeleo ya mifugo kwenye eneo husika hususani kwenye masuala ya malisho, madawa na mahitaji mengine.