Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

WAVUVI ZIWA NYASA WAKABIDHIWA MTAMBO WA KUKAUSHIA DAGAA,SOKO LA SAMAKI

Imewekwa: 25 October, 2025
WAVUVI ZIWA NYASA WAKABIDHIWA MTAMBO WA KUKAUSHIA DAGAA,SOKO LA  SAMAKI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Serikali ya elico Foundation imeikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Soko la kuuzia Samaki na Mtambo wenye Thamani ya Milioni 129.98 kwa ajili ya kukaushia Dagaa ikiwa na uwezo uliosimikwa wa kukausha mazao hayo kwa wastani wa tani 3 hadi 5 kwa siku, mradi ambao umelenga kuongeza uzalishaji wa mazao hayo yenye kuathiriwa na changamoto ya hali ya tabia ya nchi ambao ulipelekea uchakataji wa zao hilo kuwa duni.

Akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi na Kukabidhi Mtambo huo, leo Oktoba 24, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amesema Sekta ya Uvuvi imekuwa ikikabiliwa na upotevu mkubwa wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, hasa kwa dagaa ambao mara nyingi uharibika kutokana na kukaushia chini, na wakati mwingine mazao hayo hukutana na mchanga, matope, au mvua, na hivyo kupunguza ubora wake, bei yake sokoni na hata kuathiri afya za walaji.

"Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa ikiwemo mitambo ya kukaushia dagaa kwa kutumia nishati ya jua, na leo tunaenda kukabidhi mtambo wenye uwezo wa kukausha dagaa tani 3 hadi 5 kwa siku ambapo dagaa hao wanakuwa na thamani ya Milioni 10.5 hadi Milioni 17.5." alisema Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede amebainisha kuwa Miundombinu hiyo ni uwekezaji katika teknolojia rafiki kwa mazingira endelevu ya mbinu bora za uchakataji wa mazao ya uvuvi, ambazo zitaleta manufaa makubwa kwa wadau wa Sekta hiyo katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za uvuvi, kuboresha ubora na usalama wa samaki na dagaa ili bidhaa ziweze kukidhi viwango vya soko la ndani, Kikanda na kimataifa, na kuongeza kipato cha wavuvi na wachakataji wadogo pamoja na kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji.

Vilevile, Dkt. Mhede ameweka wazi kuwa wavuvi wakihakikisha bidhaa za uvuvi zinakuwa safi, bora na salama zinaweza kufungua fursa za masoko mapya, ikiwemo mataifa jirani na hata masoko ya kimataifa, na hii inatokana na Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinachangia ipasavyo kwenye uchumi shindani na shirikishi.

Pia, Dkt. Mhede, amewaweka wazi kuwa sasa Serikali imeridhia kwa kuamua siku ya leo Soko la kuuzia Samaki Mbamba Bay lianze kutumika Rasmi na amewaahidi Wavuvi  hao Vizimba vya kufugia Samaki na kuwataka wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kutumia teknolojia hiyo kwa uangalifu na umakini mkubwa, kwani ni jukumu lao kuhakikisha uwekezaji huo wa thamani unaleta manufaa ya kudumu, na Serikali itaendelea kusimamia, kutoa mafunzo, pamoja na kuweka sera na kanuni rafiki ili wavuvi na wadau wengine wa Sekta hii waweze kufaidika na rasilimali hizi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Ndg. Salumu Ismail amesema wao kama Wilaya wamepokea kwa Mikono miwili Mtambo huo na kuahidi kuutunza na kuusimamia katika shughuli zote za uzalishaji.

Ndg. Ismail, amesema teknolojia hiyo ya kisasa ya kukaushia Dagaa kwa kutumia Nishati ya jua na umeme itasaidia sana Wavuvi hasa wakati wa masika, na mazao yatakuwa salama kwani yataweza kukaushwa kwa wingi na kwa haraka zaidi.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Elico Foundation, Prof. Evelyne Mbede amesema wao wataendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na wapo tayari kuwasaidia Wavuvi nchini kote katika kuwapatia mitambo mingine ya kukaushia mazao ya Uvuvi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo