DORIA YA WAKATI MMOJA YATAJWA DHIDI YA UVUVI HARAMU

Imewekwa: Thursday 29, August 2024

DORIA YA WAKATI MMOJA YATAJWA DHIDI YA UVUVI HARAMU

Uongozi wa Mkoa wa Geita umeshauri uwepo wa doria ya wakati mmoja kwa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria ili kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi.

Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Dkt. Elfas Msenya amesema hayo (29.08.2024) alipokutana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika katika Ofisi za Mkoa wa Geita kumfahamisha lengo la timu hiyo la kuonana na baadhi ya wavuvi ili kutoa elimu juu ya uvuvi haramu.

Dkt. Msenya ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Uchumi na Uzalishaji, amesema ni vyema doria za kudhibiti uvuvi haramu katika mikoa inayozunguka Ziwa Victoria ziwe zinafanywa kwa wakati mmoja kila baada ya muda watakaokubaliana ili kuongeza nguvu kwa mikoa yote.

"Sisi kama Mkoa wa Geita tumekuwa tukifanya doria ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ninashauri kuwepo na ratiba ya pamoja kwa mikoa yote tuwe tunafanya doria kwa wakati mmoja ili kuongeza nguvu zaidi. " Amesema Dkt. Msenya

Aidha, amesema baadhi ya viongozi wa Vikundi vya Utunzaji wa Rasilimali ya Uvuvi katika Ziwa Victoria (BMU), wamekuwa siyo waaminifu katika kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi hivyo ni wakati sasa wa kuboresha namna ya upatikanaji wa viongozi wa vikundi hivyo.

Pia, amesema kuwa baadhi yao wamekuwa wakishiriki vitendo hivyo kwa kigezo cha kuleta wawekezaji kulinda maeneo ya mazalia ya samaki na kujipatia fedha kinyume na utaratibu huku wavuvi kutoruhusiwa kufika kwenye maeneo hayo.

Ili wavuvi kuondokana na zana duni za uvuvi amesema serikali ya Mkoa wa Geita imekuwa ikitoa mikopo yanye masharti nafuu ili wavuvi kuwa na zana za kisasa kwa ajili ya kuvua kwa tija na kuachana na uvuvi haramu.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mkoani Geita Bw. Mandia Kihiyo akizungumza na baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea lengo la ziara yao ya kutoa elimu kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi, hususan wavuvi dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi Ziwa Victoria, amewataka wataalamu hao kuendelea kutoa elimu na kusimamia sheria, taratibu na kanuni zlizopo ili kudhibiti vitendo hivyo.

Bw. Kihiyo amekiri kuwepo kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu katika halmashauri hiyo na kwamba wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali kukabiliana nayo ili kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inaendelea kukua na kutoa mchango wake katika ukusanyaji wa mapato.

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekuwa wakitoa elimu dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi Ziwa Victoria, kwa baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaofanya shughuli zao kwa kutegemea ziwa hilo.

.