DKT. BASHIRU-MIMI SITISHWI, NIACHENI NIFANYE KAZI YA RAIS ALIYONIPA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewaonya wanasiasa na baadhi ya watu wanaoendelea kujihusisha na kuhamasisha uvuvi usiofuata sheria maarufu kama uvuvi harama na kueleza kuwa ataendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kusimamia rasilimali za uvuvi nchini kwa maslahi ya taifa.
Kauli hiyo ameitoa Agosti 15, 2026 baada kuwatembelea wawekezaji wa viwanda vya kuchakata samaki jijini Mwanza na kuelezwa changamoto ya ukosefu wa malighafi za viwandani unaotoka na upungufu wa samaki Ziwa Victoria.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema changamoto ya ukosefu wa malighali katika viwanda vya samaki imesababishwa na uvuvi usiofuata sheria katika maziwa hususan Ziwa Victoria, nakueleza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kikosi maalum alichokiunda kimeendelea kutoa elimu kwa vitendo pamoja na kufanya utafiti kuhusu chanzo cha vitendo hivyo ambapo katika hatua za awali kimebaini kuwa kuna watu ambao wamekuwa wakijihusisha na uvuvi haramu kutokana na baadhi ya wanasiasa kuwakingia mgongo .
" Tumekubaliana na mwekezaji tutatue tatizo la malighali na hali ni mbaya sana, nilivyojaribisha kidogo kutengeneza kikosi kwa msaada wa Mheshimiwa Rais ambacho kitapita kutoa elimu kwa vitendo na kufanya utafiti wa vyanzo na mizizi ya tatizo hili, kwa hiyo niwatahadharishe waliozoea na ninawajua wote kwa majina, wengine wanajifanya wanauswahiba na viongozi wa kisiasa, sitishwi, niacheni nifanye kazi ya mheshimiwa Rais" amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Ameongeza kuwa licha ya juhudi anazozifanya za kupambana na uvuvi haramu lakini bado kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitetea vitendo vya uvuvi usiofuata sheria na akaeleza juu hatua iliyofikiwa ya kukamilisha kanuni itakadhibiti uvuvi wa samaki walio chini ya kiwango ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi Itasimamia na kulikomesha tatizo hilo.