DKT. BASHIRU AZINDUA MAABARA YA UTAFITI WA ASIDI BAHARINI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amezindua Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kwa ajili ya Utafiti wa Ongezeko la Asidi Baharini na athari zake kwa Viumbe Hai, Uzinduzi wa maabara hiyo umefanyika Leo Oktoba 09 2026 katika Makao Makuu ya TAFIRI, yaliyopo Kunduchi Jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa maabara hiyo ni sehemu ya uwekezaji katika uwezo wa Tanzania wa kulinda rasilimali za bahari, kuimarisha maamuzi ya uwekezaji katika uchumi wa Buluu na kudumisha manufaa ya kiuchumi na kijamii.
Maabara hiyo inaendeleza juhudi za Mpango wa Kitaifa na Kimataifa wa Kuongezeka kwa Asidi Baharini ulioanzishwa mwaka 2019, ambao umewezesha ukusanyaji wa taarifa kuhusu mabadiliko ya hali ya maji ya bahari na athari zinazoweza kuwakabili viumbe wa baharini.
Kupitia maabara hiyo, wanasayansi wa TAFIRI wataweza kufanya majaribio ya kisayansi ili kuchunguza athari za ongezeko la asidi baharini, sambamba na ongezeko la joto na kupungua kwa oksijeni kwenye maji kunakohusishwa na mabadiliko ya tabianchi. Tafiti hizo zitasaidia kutambua viumbe walio katika hatari zaidi na kutathmini hatua za kuimarisha ustahimilivu wao, hususani katika shughuli za ufugaji wa viumbe wa majini.