Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AWAPA SOMO WAWEKEZAJI NARCO KAGERA

Imewekwa: 02 January, 2026
DKT. BASHIRU AWAPA SOMO WAWEKEZAJI NARCO KAGERA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wawekezaji waliopo kwenye kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutumia shamba darasa la Mifugo lililopo Wilaya ya Muleba kubadili mfumo wao wa ufugaji.

Balozi Dkt. Bashiru ametoa angalizo hilo mara Januari 02,2026 wakati wa ziara yake ya kutembelea shamba hilo linalomilikiwa na mfugaji binafsi Bw. Shakiru Kyetema ambapo ameonesha kufurahishwa na mpangilio wa shughuli za ufugaji zilizopo shambani hapo hususan kwenye eneo la kilimo, uchakataji na uhifadhi wa malisho ya mifugo.

“Mkoa wa Kagera hapa tuna ranchi sita na zina maeneo makubwa kuliko hata eneo lako hili lakini wafugaji waliopewa hizo ranchi kama wawekezaji hatuoni msukumo wa kuanza mchakato wa kufuga kisasa kwa kuwa na malisho kwa hiyo nadhani baada ya hapa kuna haja kwa njia hiyo hiyo ya shamba darasa kuwaleta wawekezaji wetu” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa wawekezaji hao hawawezi kufanikisha azma yao bila kuwekeza kwenye malisho yatakayowawezesha kupata mazao bora ya Mifugo kwa upande wa maziwa na nyama.

“Kwa kuwa Jiographia ni ile ile inafanana, jitihada kama hizi hizi unazofanya hapa nadhani ziwe ndo shule kwa hao wawekezaji waje wajifunze unapopata mbegu, namna ulivyoanza, ulivyopata maji na unavyoendelea kutumia malisho haya kuanza kuzalisha ng’ombe wa maziwa” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Balozi Dkt. Bashiru amehitimisha kwa kuelekeza mikataba mipya ya wawekezaji hao iwekwe kipengele cha sharti la kuwekeza kwenye malisho ya mifugo kwa kuwa tayari ipo teknolojia, mbegu za kisasa na mifano ya kilimo cha malisho hayo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo