Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AONGEZA MSUKUMO KWENYE MAPATO UVUVI WA BAHARI KUU

Imewekwa: 17 December, 2025
DKT. BASHIRU AONGEZA MSUKUMO KWENYE MAPATO UVUVI WA BAHARI KUU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa bahari kuu (DFSA) kuongeza kiwango cha makusanyo ya mapato yatokanayo na Uvuvi wa Bahari Kuu.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo mara baada ya kufika na kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo Desemba 17,2025 visiwani Zanzibar ambapo mbali na kuwapongeza kwa kuanza kuongeza kiwango cha makusanyo amewataka kuhakikisha wanakusanya zaidi ya fedha zinazokusanywa kwenye shughuli nyingine za Uvuvi.

“Mhe. Rais hapendi michakato, anataka matokeo na nyie wenyewe mliona namna ile filamu ya Royal tour ilivyofanya mapinduzi ya sekta ya Utalii hivyo na nyie mfikirie mpango utakaofanya mapinduzi kwenye Uvuvi wa bahari kuu” Ameongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru ameitaka Mamlaka hiyo kuweka mikakati madhubuti itakayoainisha ushiriki wa sekta binafsi kwenye Uvuvi wa bahari kuu huku akizipongeza baadhi ya sekta zilizoanza kuwekeza kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ally Mohammed amesema kuwa anaamini ziara hiyo ya Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Makatibu Wakuu wa Wizara zote mbili itakuwa chachu ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyojikita kwenye kuhakikisha uchumi wa Tanzania unachagizwa kwa kiasi kikubwa na Uvuvi wa bahari kuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Salehe Yahya amesema kuwa Mamlaka yake itahakikisha inaongeza pato la Taifa kupitia uchumi wa Buluu huku akibainisha kuwa uchumi huo utaongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi mara baada ya kuanza kufanya kazi kwa Mashirika ya Uvuvi Tanzania bara (TAFICO), lile la Zanzibar (ZAFICO) na bandari ya Uvuvi inayokamilishwa ujenzi wake wilayani Kilwa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo