DKT. BASHIRU AANZA KUWAPA TABASAMU WAFUGAJI NCHINI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Damas Kamani wameanza ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya Mifugo mkoani Morogoro ambapo wametembelea shamba la Mifugo na mfugaji Maloloi Kibangashi lililopo Wilayani Movemero.
Akizungumza mara baada ya kufika kwenye shamba la Bw. Maloloi Balozi Dkt. Bashiru mbali na kuvutiwa na kasi ya mabadiliko ya mfumo wa ufugaji aliyonayo mfugaji huyo kutoka kwenye ufugaji wa asili na kugeukia wa kisasa ambapo alitoa rai kwa wafugaji wengine kote nchini kuiga mfano huo.
“Wewe ni mmoja wa wafugaji wa kisasa ambao eneo lako limepangwa, limepimwa,limelindwa kisheria, lina maji, lina malisho na lina umeme na nimeambiwa ulianza kama mfugaji wa asili wa kawaida hivyo nimekuja kukuhakikishia wewe na wafugaji wote nchi nzima kwamba Wizara yangu itakuwa na ushirikiano na wafugaji wote na mimi pia nawaomba ushirikiano” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Mhe. Dkt. Bashiru ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake inakusudia kuimarisha uzalishaji wa mifugo utakaozingatia upatikanaji wa uhakika wa malisho, maji, tiba na chanjo huku ikiendelea kuimarisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka wawekezaji wote kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanalinda fedha zote zilizotokana na kodi za Watanzania kwenye uwekezaji wao ili zitoe matokeo yaliyokusudiwa na Serikali.
“Pamoja na kwamba Mhe. Rais anaipenda sana Sekta binafsi na ametupa maelekezo mahsusi kwetu sisi wasaidizi wake kuwa lazima tuiangalie sekta hiyo kwa jicho jingine kwa sababu inaisaidia Serikali kufikisha huduma kwa wananchi wetu na kuingiza mapato hivyo ni lazima tuwe na ushirikiano wa karibu kati yetu, nyie wawekezaji na wananchi ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zozote zinazojitokeza na kazi iendelee” Ameongeza Mhe. Kamani.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Kamani walihitimisha ziara yao kwa kutembelea kituo cha ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira ambapo mbali na kuvutiwa na kinachoendelea kituoni hapo alitoa maelekezo ya kuhakikisha idara ya ukuzaji Viumbe Maji inafanya utafiti ili kuona uwezekano wa kupandikiza vifaranga vya samaki katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Ziara ya Viongozi hao itaendelea tena Novemba 27 katika mkoa wa Pwani ambapo itaanzia kwenye machinjio ya kisasa ya “Union Meat” iliyopo eneo la Ruvu.